Monday, January 22, 2018
   
Text Size

ZA KISWAHILI

  • 1
  • 2
  • 3
  • 4

Articles

Bahame asisitiza umuhimu wa wananchi kupata taarifa

HAKI

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Bahame Tom Nyanduga amesisitiza umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na haki ya wananchi kupata taarifa katika kukuza demokrasia nchini.Bw. Bahame Tom

Nyanduga aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya kuzuiwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge ijulikanayo kama Nchi yangu, Bunge Langu, Novemba 15, 2016.

“Katika nchi yenye kuamini katika demokrasia, tasnia ya habari ni mojawapo ya nguzo muhimu ya uwepo wa demokrasia ya kweli, kwani huwezesha wananchi kujua kile kinachotokea nchini, na katika jamii wakati wote kupitia uwezo wake wa kuelemisha jamii,” alisema.

Alisema Tanzania ina wajibu wa kutekeleza mikataba ya kimataifa kama ilivyoainishwa kuhusu haki za binadamu, na ndani ya Katiba ya nchi, haki ya kupata taarifa,kuwa na maoni ni haki ya msingi, kwani inawawezesha wananchi kufikia maamuzi katika masuala muhimu yanayogusa maisha yao ya kila siku.

Katika hotuba yake hiyo, Bw. Nyanduga alisema umuhimu wa kila mtu kupata habari na kuwa na maoni tofauti katika masuala ya jamii, ulitambuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1948 katika Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu.

Alisema azimio hilo linasema uhuru wa habari na maoni ni moja ya haki za msingi za binadamu, pale Azimio hilo lilipotamka kwenye Ibara ya 19 kwamba kila mtu atakuwa na haki ya kupata habari bila kubughudhiwa, atakuwa na haki ya kujieleza, kutafuta na kupokea habari, kutoa taarifa na habari, bila mipaka, kupitia matamshi, maandishi au machapisho.

Aliongeza kuwa utekelezwaji wa hayo unalenga kulinda hadhi na haki ya watu wengine, kulinda usalama wa taifa, amani na afya ya jamii na maadili.

Alisema taarifa hiyo ya uchunguzi ya kuzuiwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge, inaweza kusaidia viongozi wanaohusika na maamuzi hayo kuona ni jinsi gani uhuru wa maoni ni muhimu kuliko gharama.

“Kuna usemi usemao kwamba demokrasia siyo kitu rahisi, na ili kuijenga ni budi kuigharamia,”alisisitiza Bw. Nyanduga.

Hata hivyo alisema ameshtushwa kusoma kwenye ripoti hiyo kuwa pamoja na vyombo vya habari vya runinga kuathirika zaidi na hatua ya serikali kusitishwa kwa matangazo mubashara, lakini vyombo hivyo havi kudai haki hiyo.

Alisema badala ya vyombo vya kieletroniki pamoja na wamiliki wao kuidai haki hiyo, vyombo vya habari vya magazeti ndivyo vilikuwa mstari wa mbele kuipigania haki hiyo, huku wamiliki wa vyombo vya habari wakiwa na hofu ya kuchukua hatua kutokana na hofu waliyonayo juu ya utawala uliopo madarakani.

“Napenda niseme kwamba tasnia ya habari ni kitu muhimu sana katika jamii na nchi yoyote ile, katika kutekeleza majukumu yake. Niseme pia kwamba katika nchi yenye kuamini katika demokrasia, tasnia ya habari ni mojawapo ya nguzo muhimu ya uwepo wa demokrasia ya kweli, kwani huwezesha wananchi kujua kile kinachotokea nchini, na katika jamii wakati wote kupitia uwezo wake wa kuelemisha jamii,”alihimiza.

Bw. Nyanduga alisema ni lazima waandishi wa habari kuwa na vyanzo vya habari vinavyoaminika, na wasitoe habari za uzushi au za kubuni, ili taaluma ya uandishi wa habari iheshimike, na kuongeza kuwa huo ndiyo uweledi na umahiri pamoja na kujikita katika maadili ya kazi.

Aliongeza kuwa kwa maana hiyo wananchi hupata taarifa nyingi wakiamini kwamba taarifa au habari hizo ni sahihi, na kwamba waandishi wa habari wanafanya kazi yao kwa weledi, na kwa umakini ili kuhakikisha kuwa habari zinazowafikia wananchi zinakuwa zimefanyiwa utafiti, uchunguzi, na uchambuzi wa kutosha.

Journalism Awards

awaa

OUR RSS

  • No feeds found!