Monday, January 22, 2018
   
Text Size

ZA KISWAHILI

  • 1
  • 2
  • 3
  • 4

Articles

TAMKO LA PAMOJA KULAANI KITENDO CHA KUTEKWA NA KUPELEKWA KUSIKOJULIKANA MWANDISHI WA HABARI SALMA SAID

Tumepata taarifa za kusikitisha na kushtusha kuwa Mwanahabari Salma Said wa Zanzibar, jana alitekwa na kupelekwa mahali pasipojulikana na watu wasiojulikana na hadi sasa hivi tunavyozungumza nanyi bado haijajulikana yuko wapi. Bi Salma ni Mwanahabari anaandikia Magazeti ya Mwananchi Communications Ltd na na Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW).

Hivi karibuni Bi Salma amekuwa akitoa taarifa mbalimbali za hali ya kisiasa visiwani Zanzibar kupitia idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani na Mitandao ya Kijamii. Kwa mujibu wa Bi Salma kuandika kwake mfululizo taarifa za hali ya usalama Visiwani Zanzibar, kumepelekea yeye kupata vitisho toka kwa watu wasiojulikana mara kadhaa. Taarifa tulizo nazo ni kuwa Bi Salma alishatoa taarifa polisi.

Muda mfupi baada ya kuondoka Zanzibar taarifa zilienea kuwa Bi Salma kakamatwa na Polisi. Katika kujiridhisha tulifuatilia suala hili kwa vyombo vya usalama Visiwani Zanzibar na kupata taarifa kuwa hata Jeshi la Polisi Visiwani Zanzibar na huku bara hawana taarifa hizo. Hata hivyo, DW ilifanikiwa kumhoji Bi Salma kwa namba nyingine aliyowatumia na kupata taarifa zake kuwa alitekwa na watu wasiojulikana na kupelekwa kusikojulikana mara baada ya kutoka katika Uwanja cha Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Kitendo hiki alichofanyiwa mwanahabari huyu ni kibaya, kinakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu lakini pia kinabinya uhuru wa wanahabari na haki ya kupata habari. Hadi sasa hatujui madhila anayoyapata Bi Salma na yuko katika hali gani. Kitendo hiki kinajenga hofu kubwa miongoni mwa wanahabari na jamii kwa ujumla.

Kutokana na hali hiyo sisi wote kwa pamoja tunapenda kusisitiza yafuatayo:

 

  1. Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) , Umoja wa Klabu za wanahabari Tanzania (UPTC), Taasisi wa Wanahabari Kusini mwa Africa (Misa-Tanzania) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), kwa pamoja tunalaani vikali kitendo cha kutekwa na kupelekwa kusikojulikana kwa mwandishi wa habari Salma Said.
  2. Vyombo vyote vya usalama hasa Jeshi la Polisi vichukue hatua mara moja kumtafuta Bi Salma na kuweza kuhakikisha usalama wa mwanahabari huyu unarejea na kufuatilia kwa kina kilichomsibu.
  3. Tunawaomba wananchi wote washirikane na familia ya Bi Salma pamoja na sisi kumtafuta Bi Salma popote alipo.
  4. Tunawataka wote wanaohusika na suala hili wamwachie mara moja mwanahabari huyu aendelee na kazi zake hasa kipindi hiki muhimu cha kuelekea kwenye uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar.
  5. Tunavitaka vyombo vya usalama kuhakikisha vitisho vyote dhidi ya wanahabari na watetezi wa haki visiwani Zanzibar vinakomeshwa na kuwaacha wawe huru kufanya kazi zao katika kipindi hiki cha uchaguzi wa marudio.

Hatimaye tunapenda kuwashauri waandishi wote Visiwani Zanzibar kutopata hofu na kuacha kuandika bali waendelee kufanya kazi zao kwa umakini mkubwa na kuzingatia suala zima la usalama wao. Tunatoa tamko hili huku bado tukiendelea kutafuta taarifa zaidi kuhusu kutoweka kwa Bi Salma.

Imetolewa leo tarehe 19/3/2016 na;

 Kajubi Mkajanga, Katibu Mtendaji Baraza la Habari Tanzania

Onesmo Olengurumwa , Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania

Theophil Makunga- Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri Tanzania

Journalism Awards

awaa

OUR RSS

  • No feeds found!