Tuesday, February 20, 2018
   
Text Size

Mashindano ya EJAT kwa mwaka 2017 yazinduliwa

ejallaunch2017 thumb

Mashindano ya tisa ya Umahiri wa uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2017 yamezinduliwa rasmi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT , Kajubi Mukajanga amewataka wanahabari nchini kuanza kuwasilisha kazi zao kuanzia Oktoba 6, 2016 siku ambayo amezindua mashindano hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Baraza la Habari Tanzania (MCT). EJAT hufanyika kila mwaka.

Mukajanga katika maelezo yake alihimiza wanahabari kuwasilisha kazi zao za kushindanishwa mapema badala ya kusubiri mpaka siku za mwisho. Kazi zinazotakiwa ni za kuanzia Januari mosi had Desemba 31, 2017.

“Mashindano yako wazi kuanzia sasa na tarehe ya mwisho ya kuwasilisha kazi ni Februari 16, 2018 na siku ya sherehe ya kutoa Tuzo ni Aprili 27, 2018”, alisema.

Alisema hata hivyo kuwa idadi ya madaraja ya mashindano hayo imepungua kutoka 19 ya EJAT 2016 hadi 14 kwa EJAT 2017.

Mukajanga alifafanua kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa lengo la kuboresha ufanisi na matumizi ya raslimali.

Madaraja yaliyopunguzwa ni Kodi na Habari za Manunuzi ya Umma, Ukimwi / VVU, Habari za Uchambuzi na Matukio na Habari na Habari za Afya ya Uzazi kwa Vijana.

Mukajanga alifafanua zaidi kwamba kazi zitakazowasilishwa kwa madaraja hayo zinaweza kuangaliwa katika madaraja mengine ama daraja la wazi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Anastazia Rugaba kutoka Twaweza ambao nayo imo kwenye kamati ya maandalizi ya EJAT, aliwahimiza waandishi kuwasilisha kazi nyingi.

Alisema, tunajua kuwa mnaandika habari nzuri ambazo kwa hakika zitashinda Tuzo. Msisite na muwasilishe kazi zikiwa na habari za uhakika zenye data, aliongeza..

“Hali ya sasa ya vyombo vya habari nchini ambapo kuna sheria mbaya isiwakatishe tamaa kushiriki katika mashindano haya”, alisema.

Waandishi lazima waandike habari za uhakika zenye data na ushahidi , alisema Rugaba na kuahidi kuwa Twaweza itawasaidia kwa kuwapatia mafunzo ya habari za data ama taarifa zilizochakatishwa.

Madaraja ya mashindano hayo ni Uchumi na Biashara na Fedha, Michezo na Utamaduni, Habari za Afya, Biashara ya , Elimu, Utalii na uhifadhi, Habari za Uchunguzi, Uandishi wa Data, Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mpiga Picha Bora Magazeti, Mpiga Picha Bora Luninga, Mchora Katuni Bora, Habari za Jinsia, Wazee na Watoto na Kundi la Wazi.

Kamati ya Maandalizi ya EJAT inayoongozwa na MCT inajumuisha Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF), Taasisi ya Habari Kusini Mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-Tan), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), na Chama cha Waandishi w Habari za Mazingira Tanzania (JET).

Wengine ni Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Haki Elimu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Best Dialogue, Sikika, Agriculture Non-State Actors (ANSAF) Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya habari Tanzania (MOAT).

Mashindano hayo yalianza mwaka 2009 ambapo wanahabari kadhaa wameibuka na ushindi na kupata tuzo.

Tuzo ya Mshindi wa Maisha Katika Uandishi wa Habari (LAJA) nayo itashindaniwa mwaka huu kwa mara ya sita.

Tuzo hii hutolewa kwa mwandishi aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari.

Mwaka jana tuzo hii haikutolewa

Journalism Awards

awaa

OUR RSS

  • No feeds found!