MCT YATOA MAFUNZO YA UONGOZI KWA WAANDISHI WA HABARI VIONGOZI WANAWAKE

DODOMA 25 Mei, 2025: Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa ufadhiri wa Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo wa ViKES, linaendesha mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari viongozi, kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo Zanzibar, Jijini Dodoma. Manfunzo hayo yanahusisha washiriki 15 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Awali, akifungua mafunzo hayo, Ernest Sungura, ambaye ni Katibu Mtendaji wa MCT, amewasihi washiriki kujikita katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu jinsia na kuzungumzia matumizi ya sera ya jinsia katika vyombo vya habari. Amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea ujuzi na maarifa ya kiuongozi ili kuwasaidia katika kufanya maamuzi, na kuchakata habari zinazojumuisha jinsia.

Siku ya kwanza ya mafunzo hayo imehusisha mada ya uongozi katika vyombo vya habari, majukumu na maarifa ya kuwa kiongozi mahiri katika chombo cha habari, iliyowasilishwa na Edda Sanga, Mtangazaji nguli Mstaafu wa iliyokuwa Redio Tanzania, sasa TBC1. Mada hii pia ilichangiwa na Dk. Albert Memba, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Wakichangia matarajio yao katika mafunzo, baadhi ya washiriki wamesema kuwa wanatarajia kujifunza kuhusu mbinu za kutatua changamoto zinazowakumba wanawake katika vyombo vya habari, ikiwemo; rushwa ya ngono, usawa wa kijinsia, na ushirikishwaji katika kufanya maamuzi.

Akiwasilisha mada hiyo, huku akitoa mifano halisi ya changamoto alizowahi kupitia akiwa mtangazaji, Edda Sanga, amesema baadhi ya sifa za kiongozi mahiri mwanamke  ni; kujiamini kuwa anaweza, kuendelea kujifunza ujuzi na maarifa mapya daima, uadilifu na kuzingatia maadili ya kazi, ubunifu na uwezo wa kutambua na kutatua matatizo katika eneo la kazi.

Nao, washiriki Neema Msafiri kutoka Ebony FM, Iringa, Maryline Olotu wa KR FM, Sabra Ali wa Mjini FM, Zanzibar, na Sharon Sauwa wa Mwananchi, wakichokozwa na kuongozwa na Edda Sanga, walijadili changamoto zinazowakumba wanawake viongozi kwenye vyombo vya habari katika kukuza demokrasia na jinsia. Baadhi ya changamoto zilizoibua mjadala mkubwa ni; nafasi ya wamiliki katika kuingilia uhuru wa uhariri, kizazi kipya na ukiukwaji wa maadili ya uandishi wa habari, rushwa ikiwemo ya ngono, na baadhi ya vyanzo vya habari kushirikiana na wahariri na wamiliki katika kuzuia baadhi ya habari zisitoke. Washiriki wengine ni kutoka Radio Five ya Arusha, The Guardian Limited, Rock FM ya Mbeya, Azam Media, Habari Leo, Furaha FM, Zenj FM Radio, na Mwangaza FM.

Tangu kuundwa kwake mwaka 1995, Baraza la Habari Tanzania limeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutengeneza mazingira wezeshi kwa vyombo vya habari imara, vinavyozingatia maadili, kuwajibika kwa jamii yenya demokrasia na usawa.