Kwa Mara ya Kwanza Tuzo za EJAT kuwa Kidijitali

Baraza la Habari Tanzania (MCT) Septemba 25, 2025 limezindua mashindano ya

Tuzo za Umahiri za Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2024-2025.

Tuzo hizi zimezinduliwa sambamba na uzinduzi wa mfumo na tovuti mpya kwa ajili ya uwasilishaji kazi za waandishi wa habari zitakazoshindanishwa ambao utakuwa wa njia ya mtandao.

Akizungumza katika uzinduzi wa mashindano hayo, Katibu Mtendaji wa MCT Ernest Sungura amesema kuwa katika mashindano ya mwaka huu, kutakuwa pia na makundi mapya ya kushindaniwa.

“Kwanza nianze kuzungumzia mfumo huu mpya umeongeza ufanisi na uwazi katika mchakato wa uombaji tuzo pamoja na uchakataji wa kazi za wanahabari unaofanywa na majaji mpaka kupata washindi,” alisema Sungura akiongeza kuwa ili kuwasilisha kazi waandishi wanatakiwa kwanza kujisajili kwa kufungua akaunti kwenye tovuti hiyo.

Kwa waandishi watakaojisajili katika tovuti hii, watakuwa wanapokea taarifa zote za tuzo zitakapokuwa zinatangazwa kwa mwaka husika, lakini pia kupata mwenendo wa matokeo ya maombi ya kila mwandishi.

Tovuti hii itamwezesha mwandishi wa habari kuwasilisha kazi zake na ‘ku-save’ kidogo kidogo ili hata itakapotokea umeme umekatika, taarifa zilizojazwa hazijifuti. Pia, waandishi watakaojisajili katika tovuti hii watakuwa wanapata taarifa ‘update’ za fursa zilizopo katika sekta ya habari hapa nchini.

“Hata mchakato wa majaji utafanyika kwa kupitia mfumo huu,” aliongeza Sungura.

Katika tuzo za mwaka huu ambazo zitafanyika Disemba 2025, makundi yatakayoshindanishwa ni pamoja na Tuzo za Waandishi wa Habari Binafsi ambapo kutakuwa na kipengele cha mwandishi wa habari aliyewajibika kwa ufanisi mkubwa zaidi katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu wa 2025, Kipengele cha Mwandishi wa Habari Mbobevu na Mchambuzi Mahiri wa Mwaka.

Kundi la pili litahusisha Tuzo zinazolenga vyombo vya habari, ambapo litakuwa na vipengele kama Chombo cha Habari Kinachofuata Miongozo na Sheria, na Chombo cha Habari Kilichowajibika kwa Ufanisi Mkubwa Zaidi Kuripoti Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Kundi la tatu litahusisha Tuzo za Maudhui ya Runinga na Mtandao ambalo litakuwa na vipengele vya Maudhui Bora ya runinga ya kawaida ya mwaka na Maudhui Bora ya runinga ya mtandaoni ya mwaka.

Kundi la nne litahusisha Tuzo za Maudhui ya Picha za Magazeti na Mtandao ambalo litakuwa na kipengele cha Tuzo ya Picha Bora ya Kihabari ya Mwaka.

Kundi la tano litahusisha Tuzo za Maudhui ya Magazeti, Radio, Runinga na Mtandao ambalo litakuwa na vipengele vya Habari Bora ya Mwaka ya Maudhui ya Vijijini, Habari Bora ya Mwaka inayojumuisha video, sauti maandishi na picha (multimedia story) na kipengele cha tatu kitahusisha habari bora ya mwaka ya uchunguzi.

Kundi la Sita, litahusisha Tuzo kwa ajili ya Taasisi Zisizo za Kihabari ambapo zitakuwa na kipengele cha Taasisi iliyozingatia zaidi Haki ya Kupata Taarifa kwa Mwaka. Wakati kundi la Saba litakuwa na Tuzo ya Mafanikio ya Maisha Katika Sekta ya Habari na litakuwa na kipengele cha Tuzo ya Mafanikio ya Maisha katika Sekta ya Habari.

Mabadiliko haya ya Tuzo za EJAT yametokana na utafiti uliofanyika katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu ambao ulikuwa na lengo la kusikia mahitaji ya wadau katika kuboresha Tuzo hizo.

Kwa uzinduzi huu waandishi wa habari wa magazeti, radio, habari za mtandao (Online) na runinga wanakaribishwa kuanza kuwasilisha kazi zao kwenye Baraza ifikapo Oktoba mosi, 2025 hadi Novemba 30, 2025.