Mkutano wa Kimataifa wa Mabaraza ya Habari Afrika

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Jumamosi, 21 Juni 2025:

Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabaraza ya Habari Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 14 hadi 17 Julai 2025. Mkutano huo utafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Mgeni Rasmi aliyealikwa kufungua mkutano huo wa kimataifa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Aidha, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amealikwa kushiriki kwa nafasi ya Mgeni Maalum wa mkutano huo kushuhudia Tuzo mahsusi za Miaka thelethini (30) ya Baraza la Habari Tanzania.

Mgeni mwingine mashuhuri ni Naibu Mkurugenzi Mkuu, Mawasiliano na Habari wa UNESCO, Dkt. Tawfik Jelassi; huku tukitarajia baadhi ya mawaziri wa sekta ya habari na mawasiliano kutoka katika mataifa ya Afrika kuhudhuria. Mawaziri hao ni pamoja na Mhe. William Kabogo Gitau, Waziri wa Habari na Uchumi wa Kidijitali, Kenya, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Tanzania.

Wengine ni Mhe. Jerry Silaa, Waziri wa TEHAMA, Tanzania, Mhe. Dkt. Chris Baryomunsi, Waziri wa TEHAMA na Mwongozo wa Kitaifa, Uganda, Mhe. Cornelius Mweetwa (MB), Waziri wa Habari na Utangazaji, Zambia, Pamoja na Mheshimiwa Veronica M. Nduva, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mkutano huu unaandaliwa kwa mara ya kwanza na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (Network of Independent Media Councils of Africa—NIMCA), Umoja wa Mabaraza ya Habari ya Afrika Mashariki (East Africa Press Councils-EAPC), na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kama mshirika mahususi.

Aidha, mikutano mingine ya kimataifa itafanyika sambamba na mkutano huo, kama vile, mkutano wa East Africa Press Councils (EAPC), na World Association of Press Councils (WAPC).

Watu zaidi ya 500 (mia tano) wanatarajiwa kushiriki ambapo 150 (mia moja Hamsini) watatoka nchi mbalimbali duniani. Mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu: “Advancing Media and Communication Regulations for Journalism Excellence in Africa” (inayotafsiriwa kama “Uboreshaji wa Sheria za Habari na Mawasiliano kwa Ajili ya Umahiri wa Uandishi wa Habari Afrika”).

Kimsingi, mkutano huu ni wa mambo matatu makubwa katika siku tatu muhimu ambayo ni Kwanza: mijadala ya kitalaamu kuhusu changamoto mbalimbali zinazoathiri tasnia ya habari na namna mabaraza ya habari kote duniani yanavyokabiliana na changamoto hizo, Pili: maonesho ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia kutoka kwa baadhi ya vyombo vya habari, taasisi za umma na binafsi na Tatu: Uzinduzi wa maadhimisho ya miaka thelathini (30) ya Baraza la Habari Tanzania, ambapo wanachama wa MCT, wengi wao vyombo vya habari, taasisi za kihabari na vyuo vya uandishi wa habari watakuwa wakikumbuka na kujifunza jinsi gani walivyomudu kuzingatia weledi na maadili ya tasnia ya habari kwa kujisimamia.

Wadhamini wa mkutano huo ni pamoja na Konrad-Adenauer-Stiftung (KAS), UNESCO, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), TANAPA, PSSSF, NMB, MST, TARURA, AZAM MEDIA LIMITED, TBC, LUSH GARDEN HOTEL na KILI FAIR.

 

 

Ernest Samson Sungura

Katibu Mtendaji, Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mwenyekiti, Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA).