Dk. Mwinyi apongeza kazi za MCT

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na ujumbe wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa kazi zinazofanywa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) hususan za kutatua migogoro inayojitokeza katika sekta ya habari ni muhimu.

Akizungumza na ujumbe wa bodi pamoja na watendaji wa MCT  Ikulu ya Zanzibar, Dk Mwinyi,  Desemba 22, 2022 amesema kuwa suala la maadili na weledi katika tasnia ya habari ni muhimu kusimamiwa na wanataaluma wenyewe ikiwa ni sehemu muhimu ya kukuza  na kuimarisha tasnia ya habari kwa ujumla.

Amesema  kuwa kuimarisha na kuendeleza  uhuru wa habari ni muhimu kwa wadau kushirikiana kwa pamoja na kalamu za wanahabari zina  nguvu  kubwa kuliko silaha.

“Kulinda uhuru wa habari ni suala la muhimu kwetu sote hivyo tushirikiane katika kulinda na kuimarisha uhuru wa habari”, alisisitiza.

Akizungumzia masuala ya utafiti na majarida mbali mbali yanayochapishwa na Baraza la Habari kwa  madhumuni ya kuyatumia kukuza taaluma ya habari  alisema kuwa hiyo ni  sehemu muhimu ya kuimarisha taaluma hiyo adhimu na muhimu.

Jinsia na vyombo vya habari nalo ni suala muhimu ambalo linahitajika kuendelezwa na kuimarishwa na hivyo kutoa wito maalum kwa baraza la habari kufuatilia kwa karibu masuala ya jinsia katika vyombo vya habari.

Rais wa Zanzibar alikiri kuwa sheria za habari hapa nchini ni za muda mrefu na hivyo serikali kwa mashirikiano na wadau wa habari itaendelea kusimamia hili ili tuweze kuwa na sheria nzuri za habari hapa nchini.

 Akiwasilisha waraka maalum kutoka kwa mwenyekti wa baraza la habari, katibu mtendaji wa baraza la habari Tanzania Kajubi Mukajanga amesema kuwa moja ya majukumu ya Baraza ni kusimamia maadili na weledi ikiwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha na kuendeleza kada ya habari hapa nchini

“Majukumu ya kikatiba ya MCT ni pamoja na kusimamia maadili na kukuza weledi katika vyombo vya habari, kutetea na kushajiisha uhuru wa habari, kuhakikisha uwajibikaji wa vyombo vya habari kwa umma ikiwa ni pamoja na kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya vyombo hivyo, utafiti wa masuala ya habari, na kukuza usawa wa kijinsia katika vyombo vya habari”.

Katibu Mtendaji aliongeza kuwa ili kuifanya kada ya habari iweze kuimarika kuna umuhimu wa kuwa na sheria nzuri na rafiki kwa waandishi wa habari.

Sheria za habari za Zanzibar ni za muda mrefu na kuna vipengele kadhaa katika sheria hizo ambavyo vinarejesha nyuma uhuru wa habari na sekta habari kwa ujumla.

Alisema “tumefurahishwa na jinsi Serikali inavyowajumuisha wadau wa habari na wengine katika marejeo ya sheria hiyo ambayo imeonekana kupitwa na wakati na kukwaza uhuru wa wanahabari na vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yao na kuwapa taarifa  umma wa Wazanzibari”.

Katika mkutano huo pia Baraza la habari limepata fursa ya kumkabidhi Rais wa Zanzibar baadhi ya machapisho ya Baraza ikiwemo Kitabu cha Historia ya Vyombo vya Habari Zanzibar, Muongozo wa Kuandika Habari za Watoto, Azimio la Dar es Salaam la Uhuru wa Uhariri  na Uwajibikaji pamoja na Katiba ya Baraza la Habari Tanzania.

Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Makamo Rais  MCT,   Yussuf Khamis, wajumbe wa Bodi ya Baraza la habari Edda Sanga na Bakari machumu , Katibu Mtendaji wa Baraza la habari Tanzania Kajubi Mukajanga, afisa mdhamini wa baraza la habari ofisi ya Zanzibar Shifaa Hassan pamoja na wanachama wa MCT kutoka Chuo Kikuu cha SUZA Iman Duwe na katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar Mwinyimvua Nzukwi.