Sungura afanya mabadiliko ya utendaji MCT akitimiza siku 100
Dar es Salaam, Mei 13, 2024—Baraza la Habari Tanzania (MCT) chini ya uongozi wa Katibu Mtendaji mpya Ndugu Ernest Sungura limefanya mabadiliko ya watendaji kuimarisha utendaji katika Baraza na kuleta tija zaidi katika sekta ya habari nchini.
Baraza limeajiri Meneja wa Fedha na Utawala, Bi. Rehema Kongola kujaza nafasi iliyokuwa wazi. Bi Kongola ana cheti cha juu cha uhasibu (CPA) kutoka Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi Tanzania (NBAA). Ameanza kazi rasmi tarehe 2 Mei, 2024.
Baraza limemteua Bi. Ziada Kilobo kuwa mkuu wa ofisi ya Baraza Zanzibar na mtalaamu maalum wa uendelevu wa taasisi ambaye pamoja na majukumu mengine ataimarisha utendaji wa ofisi ya Baraza la Habari Zanzibar na uendelevu wa taasisi kwa kuongeza vyanzo vipya vya mapato yatakayolijenga Baraza.
Aidha, Bi Kilobo anatarajiwa kuboresha ufuatiliaji, tathmini ya matokeo ya kazi na uandishi wa taarifa za utekelezaji miradi mbalimbali katika Baraza. Awali, Bi Kilobo alikuwa ni meneja Rasilimali Watu na Utawala katika Baraza, nafasi ambayo imejazwa na Bi. Kongola. Bi. Kilobo anatarajiwa kuripoti katika kituo kipya cha kazi Zanzibar tarehe 27 Mei, 2024.
Katika hatua nyingine, Baraza limempandisha cheo Bi. Elizabeth Okuli kutoka nafasi ya Katibu muhstasi wa Katibu Mtendaji wa Baraza na ofisa utawala msaidizi kuwa Ofisa Rasilimali Watu na Utawala. Bi. Okuli ataanza rasmi kutekeleza majukumu yake mapya tarehe 1 Juni, 2024. Bi. SaumuMwalimu ataendelea kuwa Kaimu Meneja wa Programu za MCT.
Mabadiliko haya yamefanyika mara tu baada ya Katibu Mtendaji mpya kutimiza siku 100 ofisini. Ndani ya siku mia moja amefanikiwa kuliongoza Baraza kuandaa Kongamano la Wadau wa Habari na Uchaguzi Tanzania” lililofanyika tarehe 30 Aprili, 2024 huko Dodoma, ambalo pamoja na mambo mengine washiriki katika kongamano walijadili wajibu wa vyombo vya habari katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba. Wengine waliohudhuria ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndugu Mobhare Matinyi, mwakilishi wa Balozi wa Marekani, Uingereza nchini, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kama vile Jumuiya ya Ulaya, UNESCO, SIDA, IMS, IFES, viongozi mbalimbali kutoka vyama vya siasa wakiwemo CCM, CUF na ACT Wazalendo, wahariri na waandishi wa habari, vyama visivyo vya kiserikali na wanasheria.
Sekretariati ya Baraza la Habari Tanzania
Baraza la Habari Tanzania (MCT) lilianzishwa tarehe 30 Juni, 1995 na wadau wa Habari kwa lengo la kujisimamia katika kuhakikisha kazi za kihabari zinafanyika kwa kuzingatia ubora, maadili na weledi ili kuchangia ukuaji wa demokrasia ya Tanzania