Wadau wa habari waridhishwa na Bajeti ya Wizara ya Habari

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akiwasilisha mipango na makadirio ya bajeti ya wizara hiyo Bungeni jana Mei 16, 2024, jijini Dodoma.

Na Saumu Mwalimu

Dodoma: Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema Wizara imejipanga kuhakikisha mapinduzi ya kidigitali yanawezeshwa na TEHAMA na kuimarishwa kwa mfumo wa upashanaji habari kwa kusimamia uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Ameongeza kuwa Wizara pia imejipanga kukamilisha maboresho ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003, na kutengeneza mkakati wa ulinzi wa watoto dhidi ya ukatili mtandaoni.

Waziri Nape ameyasema hayo leo Mei 16, 2024 wakati akisoma bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (MICIT), ambapo jumla ya TZS 181 bilioni zimeidhinishwa na Bunge kwa ajili ya shughuli za maendeleo na matumizi ya kawaida ya Wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025.

Wadau wa habari likiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT), ambalo liliwakishwa na Kaimu Meneja Programu, Saumu Mwalimu, wameshudia kusomwa kwa Bajeti hiyo ambayo imekonga nyoyo za wadau wa habari nchini.

Wadau wengine waliohudhuria shughuli za usomwaji wa Bajeti hiyo ni pamoja na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), JamiiForums, JOWUTA, Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), vyombo vya habari na waandishi wa habari.

Baada ya kusomwa kwa Bajeti hiyo, wadau wa habari walikua na maoni yafuatayo juu ya bajeti hiyo. Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Kenneth Simbaya alisema bajeti ya mwaka huu ni ‘progressive’ inayotia matumaini ukiangalia pamoja na mipango iliyowekwa.

“Ukilinganisha na bajeti zilizopita, kuna mambo unayaona ni ya tofauti katika bajeti hii, japokua bado yapo yale ambayo yameendelea kuwepo katika kila bajeti, ninaamini, kama mipango iliyowekwa itatekelezwa itasaidia kuiboresha sekta ya habari.

“Waziri amekua akirudia mara kwa mara kwamba waandishi wa habari chini ya Rais Samia Suluhu Hassan wapo salama, tusingependa usalama huo uwe ni utashi wa kiongozi, bali mifumo inayowekwa ambayo hata akija kiongozi mwingine, waandishi waendelee kuwa salama,” alisema.

Simbaya alisisitiza kwamba Wizara iendelee kuitazama sekta binafsi zikiwemo asasi kama mdau muhimu katika kutimiza malengo ya Wizara yake. “Na nitoe wito kwetu sisi wadau, pale tunapoona tunaweza kuisaidia serikali iwe kwa mali ama mawazo tufanye hivyo, kwa sababu mafanikio hayaletwi na mtu au taasisi moja,” aliongeza Simbaya.

Naye mwandishi wa habari na mtangazaji mkongwe, Rose Haji alisema katika historia yake ya kufuatilia bajeti, hii ndio bajeti ya kwanza ambayo imetambua umuhimu wa vyombo vya habari, mwandishi wa habari na habari katika nchi.

Alisema kwamba kwa Wizara na hata wabunge kujadili kuona namna gani inaweza kujipanga na kuweka kiasi cha fedha kwa ajili ya wanahabari, inaonyesha ukuaji wa thamani wa kada hiyo.

“ Tumeshuhudia Bunge likitoa ‘due respect’ kwa habari, vyombo vya habari na hata mwandishi, wabunge wamejadili kuhusu suala ya uchumi wa vyombo vya habari kwa mfano, yamejitokeza mapendekezo kadhaa wakiitaka Wizara  kuweka angalau asilimia fulani ya bajeti yake kwa ajili ya maendeleo ya vyombo vya habari sambamba na kuhakikisha Wizara hiyo inasimamia ulipwaji wa madeni ambayo yamekuwepo kwa zaidi ya miaka saba,” alisema Rose Haji.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Selemani Msuya alisema hotuba imeonyesha mwelekezo mzuri na kushauri kuwepo kwa mifumo ya kisheria itakayolinda sekta hiyo na sio kutegemea hisani ya kiongozi aliyepo madarakani.

“Waziri ameeleza walivyojipanga kutatua changamoto za sekta ya habari ikiwemo kulipa madeni na waandishi wa habari kupata mikataba ya ajira hilo haliwezi kufanyika kwa kuamini utashi wa Rais Samia Suluhu Hassan pekee, bali mifumo inatakiwa kupewa nafasi,” alisema.

Aidha amezishauri taasisi za kihabari kushirikiana katika kupigania maslahi ya waandishi wa habari ambao wengi wanapitia wakati mgumu kichumi, kijamii na kikazi.

Akizungumzia suala la uhuru wa kujieleza kama lilivyotajwa kwenye bajeti ya Wizara, Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums Maxence Mello amesema Serikali imefurahishwa na ripoti ya Reporters Without Boarders, kwa sababu tumepanda viwango, lakini tumepanda kwa utaratibu gani.

“Tanzania iliwahi kuwa nafasi ya juu zaidi ya 97, nadhani tuliwahi kuwa ya 65 miaka ya nyuma, sasa tumefikaje hadi 143 hadi tuishangilie hii ya 97 ni kwamba hatusikilizani, ni kama tunagombea fito wakati tunajenga nyumba moja” alisema.

Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya wadau wa ndani ya sekta ya umma, asasi za kiraia na sekta binafsi katika kujenga uwanja mpana na kuilinda Ibara ya 18 na kuhakikisha uhuru wa kujieleza unadumishwa, vyombo vya habari vinalindwa, kwa mujibu wa sheria na taratibu tulizojiwekea na sio tulizowekewa.