SMZ yaombwa Sera na Sheria za Habari Zanzibar

Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar (ZBC), Suleiman Abdalla, akitoa hotuba yake wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Zanzibar, Mei 23, 2024, katika ukumbi wa ZSSF uliopo Kariakoo, Zanzibar.

 

Zanzibar: Baraza la Habari Tanzania (MCT), limeiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa majadiliano ya kutaka mabadiliko ya Sera na Sheria za Habari Zanzibar yawe ya mwisho na ibaki kwa wadau kupata Sera na Sheria nzuri.

Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura ameyasema hayo leo Mei 23, 2024 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Social Security Fund (ZSSF), mjini Zanzibar, Mei 23, 2024.

“Tunaiomba serikali kufanya mabadiliko ya Sheria na Sera za Habari Zanzibar na majadiliano ya kutaka mabadiliko hayo yawe ya mwisho tupate sheria na sera nzuri, tunataka kuona vitendo maana muungwana ni kitendo,” alisema Sungura.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Uhuru wa Vyombo vya Habari na Mageuzi ya Sera na Sheria za Habari Zanzibar”

Naye Mwenyekiti wa Zanzibar Press Club (ZPC), Abdallah Mfaume alisema kauli mbiu ya kitaifa imejikita katika suala la mazingira, lakini ili kujikita katika uandishi wa habari mahususi, tunahitaji sheria na sera ambazo zitawahakikishia waandishi wa habari uhuru na usalama wao.

“”Kauli mbiu ya Kitaifa imejikita katika mazingira lakini tunahitaji sheria na sera ambazo zinaweza kutuhakikishia uhuru wetu na usalama  wetu ili tuweze kufanya kazi ya uandishi kwa weledi” Mwenyekiti wa ZPC.

Naye Makamu wa rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Yusuph Hamisi Yusuph alisema Tanzania haina waandishi wa habari kwa sababu tasnia ina wahariri ambao hawawezi kuandika intro.

” Sasa hivi Tanzania haina waandishi wa Habari, maana tuna wahariri wa Habari ambao hawawezi hata kuandika intro, waandishi wamepoteza ari ya kujifunza, waandishi wanavyeti vinavyowafanya wawe wahariri,” alisema Makamu wa rais wa MCT.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Suleiman Abdalla alisema Serikali imekusudia kuvizawadia vyombo vya habari ambavyo vimefanya vizuri kwa mwaka mzima bila kukizana na sheria, pamoja na kuanza kutoa udhamini kwa makongamano ya aina hii.

Aliwataka waandishi wa habari kujikita zaidi kwenye uandishi wa habari unaozingatia maadili na taaluma ya habari, na kuwataka kuacha uandishi wa habari wa mihemuko.

Maadhimisho ya siku ya uhuru wa Habari yameratibiwa kwa ushirikiano wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Zanzibar Press Club (ZPC), Tanzania Media Women Association – Zanzibar, WAHAMAZA na Common Wealth Foundation.