Na Tumbi Kiganja
Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Jaji mstaafu Benard Luanda amevitaka vyombo vya habari na Wandishi wa habari kuwa makini katika utendaji kazi wao wa kila siku ili kuepukana na sheria ambazo bado zinaonekana kuwa kikwazo kwao.
Kauli hiyo ameitoa Oktoba 4, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa alipotembelea vyombo vya habari vya Jamhuri media, Azam Media, Mwananchi Communications Limited Pamoja na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC).
Jaji Luanda amesema kuwa vyombo vya habari ni muhimili muhimu sana katika jamii hivyo ni muhimu kuchapisha au kutangaza habari za kweli na zilizofanyiwa utafiti wa kina ili kupunguza misuguano baina ya vyombo hivyo na jamii au serikali.
“Kuna sheria nyingi sana ambazo zinagusa tasnia ya habari na nimeona mara kadhaa sheria hizi zikitumika kufungia vyombo vya habari hasa pale mamlaka inapokuwa na mtazamo kuwa kilichotangazwa au kuchapishwa kina athari kwa njia moja au nyingine, ingawa kwa upande wenu ninyi mnaona mko sawa” alisema Jaji Luanda.
Jaji Luanda aliongeza kuwa ni vyema kwa vyombo vyote vya habari nchini kuhakikisha vinafanya kazi zake kwa kuzingatia misingi ya uandishi wa habari ili kupunguza madhara ya kupigwa faini, au kufungiwa.
Kwa upande wa katibu mtendaji wa Baraza, Ernest Sungura amesema kuwa ni muhimu wanahabari tujitenganishe na uanaharakati, kwani kwa kufanya hivyo vitajenga heshima na kuendelea kuaminika na jamii.
“Tasnia yetu ya habari ina miongozo ya kutosha hivyo lazima tujisimamie na tusikubali kuingiliwa na wanasiasa sababu wao wana agenda zao wakati sisi kama muhimili usio rasmi, agenda yetu kuu ni kufanya kazi kwa ajili ya jamii”, Alisema Sungura.
Nae Afisa Mwendeshaji mkuu wa Azam Media, Yahya Mohamed alisema kuwa yeye ana imani kubwa sana na Baraza la Habari Tanzania na yuko tayari kushirikiana na Baraza muda wowote, si kwenye masuala ya tuzo za EJAT pekee bali kwenye miradi mingine yeyote itakayojitokeza.
“Azam Media tunajua kuwa MCT ni chombo chetu hivyo lazima tukipe ushirikiano wa aina yoyote ili kuhakikisha ile dhana ya kujisimamia (self regulation) iweze kuonekana dhahiri kuanzia kwa wadau na wanachama wa MCT” aliongeza Yahaya Mohammed.
Mhariri mtendaji wa gazeti la Jamhuri alilishukuru Baraza kwa kumpa heshma kuwa chombo cha Habari cha kwanza kutembelewa na rais mpya wa MCT, huku akitoa pongezi kwa Katibu Mtendaji kwa kuimarisha ushirikishwaji wa wadau na wanachama. “Binafsi nafurahi sana kuona kuwa umeongeza ukaribu zaidi kati ya Baraza na wanachama wake, hongera sana Katibu “
Ziara hii pia iliweza kukutanisha timu ya MCT na uongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communications ambao hivi karibuni wamekutana na adhabu ya kufungiwa kwa siku 30 kutochapisha aina yoyote ya maudhui katika mtandao wao wa Mwananchi digital. MCT ilisikiliza changamato zao na kushauri baadhi ya mambo ambayo wanaweza kuyafanya kwa sasa na kwa baadae pia ili kuepukana na changamoto zilizowakuta.
Ziara hii pia ilihusisha kuona namna gani vyombo hivi vimefanya uwekezaji wa vifaa mbalimbali na tekinolojia za kisasa ili kuweza kufikisha Habari kwa jamii.
Kwa upande wa TBC, timu ya MCT ilipokelewa na Mkurugenzi wa habari na matukio wa TBC, Eshe Muhiddin ambae alisema kuwa MCT ni chombo muhimu kwani kimekuwa kikisimamia maadili ya uandishi wa Habari hasa kwa kutoa miongozo mbalimbali.
Eshe alisisitiza kuwa serikali imeendelea kuwekeza kwenye shirika hilo huku akiwaonyesha baadhi ya vifaa vya kisasa vilivyofungwa kwa ajili ya kuhakikisha jamii inapata taarifa kwa wakati.
Katibu Mtendaji alitoa shukurani kwa viongozi wote wa vyombo ambavyo vilitembelewa na MCT huku akisisitiza kuwa ziara hizo zitaendelea kwa vyombo vingine vya habari vilivyopo ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam.