Waziri Mkuu Majaliwa: Akili Mnemba Siyo Kikwazo, Awaasa Waandishi Nchini

Arusha: April 29, 2025

Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa amewataka wanahabari nchini kutumia Akili Mnemba katika kutekeleza majukumu yao na kwamba wasiione kama kikwazo. Pia amewataka kuwekea mkazo maadili, habari za ujasiriamali na utamaduni.

Waziri Mkuu, ambaye amekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yaliyofanyika jijini Arusha, April 28-29, 2025, kwenye hoteli ya Gran Melia, amewasisitiza washiriki kujadiliana kwa kina kuhusu masuala hayo.

Amesema, maadili ni muhimu katika kulinda heshima ya vyombo vya habari, wakati mambo ya ujasiriamali ni muhimu katika kuishawishi jamii kuimarisha uchumi wake, na utamaduni ndiyo roho ya taifa.

Amesisitiza kuwa mijadala inapaswa kujikita katika namna ya kuonesha mafanikio ya serikali hususani mchango wake katika kuendeleza sekta ya habari. Ameahidi kwamba, serikali itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari na inatambua umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari kwa taifa.

Pamoja na kupongeza maadhimisho hayo, Waziri Mkuu, amewahimiza wanahabari kujadili mahitaji ya mabadiliko ya sera na sheria mbalimbali za habari,
ambazo, amesema, serikali ipo tayari kupokea maoni hayo na kuyafanyia kazi kwa maendeleo ya tasnia ya habari nchini.

Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu; Uhabarishaji kwenye dunia mpya: Mchango wa Akili Mnemba kwenye uhuru wa vyombo vya habari, inayotoa changamoto kwa waandishi, wamiliki wa vyombo vya habari na serikali kujadili namna Akili Mnemba inatumika katika kuibua fursa kwa uhuru wa vyombo vya habari huku ikisaidia haki ya watu kupata habari sahihi.

Awali, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa Akili Mnemba isiwadumaze waandishi wa habari na badala yake iwe nyenzo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewapongeza wanahabari kwa kuendelea kuandika habari zenye maslahi kwa ya jamii.

Katika ushiriki wake kwenye maadhimisho hayo, Baraza la Habari Tanzania (MCT), likiongozwa na Katibu Mtendaji, Ernest Sungura na baadhi ya wafanyakazi wa Baraza, liliwashirikisha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Kituo cha Sheria na Haki za Binanamu (LHRC), katika kuandaa mjadala maalumu, ulioshirikisha Bunge la Tanzania, katika kujadili Mfumo wa Kisheria na Udhibiti na Wajibu wa Bunge Katika Uhuru wa Vyombo vya Habari nchini.

#WPFD2025 #AI #AIandMedia
#jamiiforums #swedenintz #MCT@30
#ofisiyawazirimkuu #wizarahmth