Azory Gwanda aongoza orodha ya walioathirika na tisho la vyombo vya habari duniani

Azory Gwanda,  mwanahabari wa kujitegemea wa Tanzania aliyetoweka kwa zaidi ya miezi 18 anaongoza  orodha ya  walioathirika na tishio  kwa vyombo vya habari kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na  Umoja wa vyombo huru  vya habari  wa One Free  Press Coalition.

Nick Turner  wa   Bloomberg News aliripoti Juni 3,2019 kwamba orodha ya dharura ya mwezi  inajumuisha  pia suala la   mwanahabari wa  Washington Post,   Jamal Khashoggi, aliyeuawa katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia  mjini Istanbul,  Uturuki  mwezi Oktoba mwaka jana. Mauaji hayo hayajafanyiwa uchunguzi  huru na Umoja wa Mataifa, kundi hilo limeeleza.

Bloomberg News  ni miongoni mwa  vyombo vya habari, ikiwemo BuzzFeed  na  Washington Post  vilivyojiunga na Umoja  huo wa  One Free Press Coalition mwezi uliopita. Mashirika ya habari ya  Associated Press, Reuters  na gazeti la  Financial Times   ni sehemu ya umoja huo unaolenga kuinua uelewa  kuhusu  vitisho dhidi ya  uhuru wa habari duniani kote.

Gwanda aliyekuwa akiandikia  kampuni ya  Mwananchi Communications, wachapishaji wa magazeti ya  Mwananchi  na The Citizen newspapers kutoka Kibiti  Kibiti, Mkoa wa Pwani alitoweka tangu Novemba 2017  na serikali ya Tanzania  bado haijaeleza  kuhusu wapi alipo.

Wadau wa habari  nchini wakiongozwa na  umoja wa Haki  ya  Kupata Taarifa (CoRI)  inayoongozwa na Baraza la habari Tanzania (MCT) wameanzisha  jitihada za kukusanya saini  kwa lengo la kushinikiza  serikali kuchukua  hatua za kumtafuta Gwanda na kueleza matokeo yake kwa umma.

Hii hapa ni orodha ya dharura muhimu  kwa mwezi Juni:                           

  1. Azory Gwanda, mwandishi wa kujitegemea wa Tanzania aliytoweka tangu Novemba 2017. Alikuwa akichunguza habari za mauaji katika eneo alilokuwa akifanyakazi.
  2. Jamal Khashoggi, alieuawa katika Ubalozi mdogo wa Saudi Arabia ulioko Istanbul, Uturuki.
  3. Aasif Sultan, mwandishi wa Kashmir Narrator aliyekamatwa kwa tuhuma dhidi ya serikali Agosti   2018.
  4. Claudia Duque, mwandishi wa Colombia anayenyanyaswa kwa  miaka kadhaa.
  5. Miguel Mora na Lucía Pineda wa  gazeti la 100% Noticias  la nchini Nicaragua  ambao wameshikiliwa kwa zaidi miezi mitano kwa tuhuma   za kuchochea “ chuki na vurugu”.
  6. Truong Duy Nhat, mwanamtandao wa Radio Free Asia ambaye ametoweka tangu Januari, Bangkok, Thailand.
  7. Sevinc Osmanqizi,anayenyanyaswa na kituo cha runinga cha Real TV kinachounga mkono serikali ya Azerbaijani.
  8. Abderrahmane Weddady na Cheikh Ould Jiddou, wako gerezani tangu Machi nchini Mauritania kwa tuhuma ya kusambaza habari zisizo za kweli. 
  9. Seyoum Tsehaye, aliyekamatwa baada ya serikali ya Eritrea  kupiga marufuku vyombo vya habari bianfsi  mwaka 2001. 
  10. Mina Karamitrou, mwandishi wa polisi kwa Idara ya Kigiriki ya  CNN ambaye alipigwa na  bomu lililotegwa kwenye gari.