Maadhimisho ya Siku ya Kukomesha Vitendo vya Ukatili kwa Waandishi wa Habari Novemba 2, 2022

Dar es Salaam, Novemba 2, 2022

Maadhimisho ya siku ya kukomesha na kuondosha kabisa vitendo vya ukatili kwa waandishi wa habari (International Day to End Impunity for Crimes against Journalists) ni siku muhimu hasa ikizingatiwa kuwa sekta ya habari ni moja ya nguzo muhimu za kuimarisha demokrasia, utawala bora na uwajibikaji, ambavyo ni vigezo muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi.

Siku hii imekuwa inaadhimishwa Novemba 2 kila mwaka kufuatia uamuzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutokana na vitendo vilivyoenea katika nchi mbali mbali duniani, ambapo waandishi wa habari wanakabiliwa na changamoto ikiwemo hata kupoteza maisha wakati wa kutekeleza kazi zao, na madhila haya yakiachwa bila uchunguzi wa kina na wahusika kuchukuliwa hatua.

Kazi hii imekuwa ni chanzo cha maafa makubwa kwa wanaotekeleza kazi zao na ndio maana kukawa na haja ya kuweka siku maalum ili kwa pamoja duniani tutafakari madhila na maafa wanayokumbana nayo waandishi wa habari pale wanapotekeleza majukumu yao, na hatua zinazochukuliwa kukomesha hali hii.

Takwimu za dunia zinaonyesha kuwa katika nusu muongo uliopita ni asilimia 13% tu ya kadhia za madhila dhidi ya wanahabari, ikiwamo mauaji, ndio zilifikia mwisho wake; nyingi ya kesi hizo bado zinaendelea kudorora bila ya kufikiwa ufumbuzi.

Aidha, waandishi wanawake wamekuwa wakipata vitisho mahsusi na mashambulio ya mwili na ya mtandaoni wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Utafifi wa UNESCO unaonyesha kuwa asilimia 73% ya waandishi wanawake wamekuwa wakikabiliwa na vitisho vya aina mbali mbali wakiwa kazini.

Waandishi wamekuwa wakipata madhila mbalimbali ikiwemo kudhalilishwa, kuonewa, kushambuliwa, vitisho vya kuhatarisha usalama wao na hata kuuliwa, mambo ambayo yamekuwa yakiwaathiri si kimwili tu bali hata kiakili.

Hapa nchini nako kumekuwa na vitisho kwa waandishi, kupigwa na baadhi ya wakati kunyang’anywa au kuharibiwa vifaa vyao vya kazi wakati wakitekeleza majukumu yao.

Wakati huu wa maadhimisho haya tunakumbuka kwa masikitiko makubwa kupotea kwa mwandishi wa Mwananchi Azory Gwanda ambaye amepotea tokea Novemba 2017 na hadi hivi sasa hakuna maelezo yoyote kuhusu kutoweka kwake.

Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Habari Tanzania katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka 2022 kuna matukio ya madhila 11, ambayo yametokea.

Matukio ambayo Baraza limeyarekodi kwenye kanzidata yake katika kipindi hicho ni pamoja na ya vyombo vya habari kufungiwa, wanahabari kunyanyaswa, kukamatwa, kunyimwa taarifa na kutishiwa.

Madhila yamekuwa yakipungua miaka ya hivi karibuni, ambapo kipindi kama hiki mwaka jana kulikuwa na madhila 14.

Kwa mujibu wa kanzidata ya MCT, mwaka 2020 kulikuwa na matukio ya ukiukwaji wa haki za waandishi wa habari 43 wakati mwaka 2021, ilirekodi matukio 25.

Hata hivyo, pamoja na kupungua huko, ni lazima tukumbuke kuwa bado hadi hivi sasa kuna sheria kadhaa kandamizi ambazo zina vipengelee ambavyo vinarejesha nyuma uhuru wa habari na vinawafanya waandishi wa habari kutokuwa na mazingira bora ya kufanyia kazi zao.

Baadhi ya sheria hizo ni pamoja na sheria Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, sheria ya Takwimu, sheria ya Makoza ya Mtandao na nyingine ambazo bado zinakwaza uhuru wa habari na kuwafanya waandishi wa habari wafanye kazi zao katika mazingira magumu.

Serikali imeanzisha mchakato wa kurekebisha sharia ya Huduma za Vyombo vya Habari na tunaipongeza sana.

Pamoja na kupongeza tunasisitiza kuwa wadau lazima watambue kuwa bado uhuru na mazingira ya habari yapo kitanzini na waendelee kusisitiza mchakato shirikishi wa marekebisho.

Takwimu za dunia za Press Freedom Index zinaonyesha kuwa Tanzania tupo katika namba 123 kwa mwaka huu 2022 wakati katika kipindi cha 2021 tulikuwa wa 124. Hii sio hali ya kujivunia.

Kwa kupitia maadhimisho haya ya kupinga ukatili dhidi ya waandishi wa habari tunatoa wito maalum kwa Serikali kuzingatia kwa kina suala la kuyafanya mazingira ya habari kuwa rafiki ili waandishi wa habari waweze kufanya kazi zao kwa umahiri, weledi na kutumia kalamu zao bila hofu wala woga kwa lengo la kuimarisha demokrasia, uwajibikaji na kushajiisha maendeleo endelevu hapa nchini.

Wakati huu Baraza la Habari likihimiza mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa waandishi wa habari pia tunawakumbusha waandishi nao kuzingatia umahiri na kufuata maadili ya kazi yao.

Kwa kumalizia tukumbuke kuwa uhuru na ufanisi katika vyombo vya habari ndio kielelezo cha demokrasia halisi. Kulinda usalama wa wanahabari na vyombo vyao ni kuilinda demokrasia.

 

Kajubi D. Mukajanga

Katibu Mtendaji