TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 Lindi, Novemba 02, 2023

Baraza la Habari Tanzania (MCT) kama ilivyo ada linaungana na dunia katika kuadhimisha siku ya kukomesha na kuondosha kabisa vitendo vya ukatili dhidi ya waandishi wa habari (International Day to End Impunity for Crimes Against Journalists).

Siku hii ni muhimu na adhimu hasa ikizingatiwa kuwa waandishi wa habari ni nguzo muhimu ndani ya vyombo vya habari katika kuimarisha demokrasia, utawala bora na uwajibikaji ambapo ni vigezo muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi.

Kila mwaka siku hii imekuwa inaadhimishwa kutokana na vitendo vinavyoenea katika nchi mbali mbali duniani.  Katika kila sehemu bado waandishi wa habari wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kupoteza maisha wakati wa kutekeleza kazi zao.

Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu, MCT kupitia kanzidata yake limerekodi madhila 21 ya waandishi wa kufanyiwa vitendo ama vinavyozuia kupata taarifa au vinavyofanya aogope kutimiza majukumu yake kama mwandishi wa habari.

Madhila hayo ni pamoja na kunyimwa taarifa matukio (8), vitisho (5), kukamatwa (3), mashambulizi (2), na udhalilishaji (3).

Mwaka huu matukio ya kunyimwa taarifa yamekuwa mengi zaidi ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita, ambapo mwaka 2022 kulikuwa na matukio matatu, 2021 matukio manne na 2020 matukio mawili.

Baraza limegundua kuwa bado kuna tatizo katika utoaji wa taarifa, pamoja na maelekezo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoyatoa Machi 27, 2023 katika kikao kazi cha 18 cha maafisa habari, uhusiano na mawasiliano wa umma, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu aliziagiza Wizara, Taasisi za Umma na Idara za Serikali kutenga bajeti kwa ajili ya kugharamia shughuli za utoaji taarifa kwa wananchi, kwa usahihi na kwa haraka.

Mbali na agizo hilo kukiukwa tumeona baadhi ya maafisa wakitoa maamuzi ambayo yanakwenda kinyume na sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ya mwaka 2016, kwa kuwalazimisha watafuta taarifa kwenda Tamisemi kupata barua ya kuwaruhusu kwenda kuomba taarifa katika halmashauri.

Matukio matano yamezihusisha halmashauri za wilaya za Mpwapwa, Muleba, Kilosa, Njombe na Halmashauri ya Mji wa Ifarakara. Ambapo katika tukio la Ifakara, ilibidi Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali kulitolea maelekezo.

Eneo jingine ambalo Baraza imekutana nalo mwaka huu, ni suala la Mkataba wa Bandari.  Katika suala hilo Baraza limerekodi matukio yafuatayo, kunyimwa taarifa zilizohusiana na mkataba wa bandari tukio moja, vitisho matukio mawili na kukamatwa na baadaye kutakiwa kujieleza matukio mawili.

Matukio hayo hapo juu yalihusu kukamatwa kwa waandishi ambao walirusha maoni ya kuupinga mkataba wa bandari, wengine walizuiwa kufanya kipindi kilicholenga kuujadili mkataba huo, na mwingine kutakiwa kujieleza polisi.

Kwa mwaka huu kauli mbiu ni madhila dhidi ya waandishi wa habari, uadilifu wa uchaguzi, na jukumu la viongozi wa umma (Violence against journalists, the integrity of elections, and the role of public leadership):

Waandishi wa habari na vyombo vya habari hutimiza jukumu muhimu katika jamii, kudumisha na kuwezesha demokrasia na kushikilia mamlaka ya kuwajibika. Ni muhimu kwa taasisi imara na zinazowajibika na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Lakini nafasi hii muhimu inawaweka waandishi wa habari katika hatari. Kujitolea kwao kuchunguza na kufichua ukweli kunamaanisha mara nyingi wanalengwa kwa mashambulizi, kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria, na hata kifo.

Kupitia siku hii Baraza linapenda kuwakumbusha waandishi wa habari kuwa mwakani, Tanzania inaingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, waandishi mnatakiwa kuwa makini katika uandishi wenu.

Katika chaguzi zijazo kutakuwa na taarifa zinazoandaliwa na akili bandia, kutakuwa na fake news na pia kutakuwa hate speech. Ni jukumu la kila chombo cha habari kujiandaa kutoa mafunzo kwa waandishi wake juu ya namna ya kugundua hizo aina mpya za upotoshaji.

Waandishi wa habari msiwe chanzo cha kusambaza taarifa ambazo siyo za kweli au ambazo hazijathibitishwa kutoka kwenye vyanzo sahihi ili kuiepusha nchi kuingia katika taharuki.

Katika Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari, tunatoa wito:-

Kwa Serikali

Kutengeneza mazingira rafiki ya utendaji kazi kwa waandishi wa habari ikiwa ni pamoja na ya upatikanaji wa taarifa pamoja na uhuru wa kujieleza kwa wananchi, taasisi na vyombo vya habari;

Kuwachukulia hatua wale wote wanaozuia ama kukwamisha utendaji kazi wa waandishi wa habari katika upatikanaji wa taarifa katika ofisi za umma kinyume cha sheria.

Kusimamia suala la upatikanaji taarifa kwa haraka na kwa usahihi, na kuhakikisha wakurugenzi wa halmashauri za wilaya wanatimiza maelekezo ya Waziri Mkuu.

Kuwawekea mazingira salama ya kufanya kazi zao waandishi wa habari na kuwafikisha mahakamani wale wanaofanya uhalifu dhidi ya waandishi.

Waandishi wa habari

Kufanya kazi kwa weledi mkubwa, kufuata maadili na miongozo ya uandishi wa habari katika kazi zao za kila siku.

Kuchukua tahadhari hasa ya mabadiliko ya teknolojia ili kuepukana na taarifa za uongo.

Kuendelea kuomba taarifa kwa kufuata sheria inavyoelekeza.

Kwa Jamii

Ombeni taarifa mbali mbali katika maeneo yenu ili kupata haki zenu, pale mnapo nyimwa taarifa, msisite kuripoti katika taasisi husika juu ya kunyimwa taarifa.

 

Kajubi D. Mukajanga 

 

Katibu Mtendaji