Wakati Serikali ikizindua Bodi ya Ithibati

  • MCT yasisitiza umuhimu wa Sheria ya MSA 2016 kufanyiwa marekebisho

Na Paul Mallimbo

Wakati Serikali ikizindua Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeendelea kuhimiza umuhimu wa Serikali kuifanyia marekebisho Sheria ya Huduma za Habari, kuheshimu maamuzi ya Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) na kuifanyia marekebisho Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003, ambayo imepitwa na wakati.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania Ernest Sungura, alikuwa mmoja wa wazungumzaji katika shughuli ya uzinduzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) leo Machi 3, 2025, jijini Dar es Salaam.

Alisema MCT ilifungua kesi dhidi ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari (MSA) katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), ambapo hukumu ilitolewa Machi 28, 2019 ikielekeza vifungu kadhaa vya sheria hiyo vifanyiwe marekebisho.

Mahakama ilisema kuwa vifungu hivyo vinakiuka Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu vinadhoofisha uhuru wa kujieleza, na kwamba baadhi ya vifungu hivyo havijapita kipimo cha kisheria cha viwango vitatu (three-tier test).

Sungura alisema japo ni miaka mitano imepita tangu hukumu hiyo itolewe, bado MCT inaamini serikali itarejea katika hukumu hiyo na kuzingatia marekebisho pendekezwa muhimu ya sheria kwa manufaa ya tasnia ya habari nchini.

Naye mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema kuteuliwa kwa wajumbe hao wa Bodi, kumetokana na mahitaji makubwa ya tasnia ya habari.

Alisema kutokana na ongezeko la waandishi wa habari, Serikali iliona kuna umuhimu wa kuwa na chombo kitakachosimamia sekta hii katika maeneo ya maadili, weledi, ukweli na uwajibikaji.

Waziri kabudi alitoa maagizo saba kwa Bodi hiyo ambayo ni kuhakikisha waandishi wa habari wote wanazingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia taaluma. Ithibati ya wanahabari itasaidia kuondoa uandishi usio wa kimaadili na kuongeza heshma ya taaluma ya habari.

Alisema Bodi inapaswa kuanza kwa kuwalea na kuwapa miongozo mbali mbaliĀ  juu ya taaluma yao na baadaye kuchukua hatua stahiki. Bodi inapaswa kuandaa na kusimamia utaratibu wa kusajili wa waandishi wa habari kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma. Mfumo huu unapaswa kuwa shirikishi, na unaoendana na maendeleo ya kiteknolojia na mazingira ya sasa ya sekta ya habari.

Prof. Kabudi katika agizo lake la tatu alisema Bodi ina jukumu la kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanazingatia maadili ya taaluma kwa kupewa miongozo na mafunzo ya mara kwa mara. Kuwa na utaratibu wa kushughulikia malalamiko na ukiukwaji wa maadili kwa haki na uwazi.

Aliiagiza Bodi hiyo kuwa haina budi kushirikiana na vyombo vya habari, vyuo vya mafunzo ya uandishi wa habari, na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanapata mafunzo ya mara kwa mara na kuwa na ujuzi wa kisasa.

Waziri Kabudi aliagiza kuandaliwa kwa programu za uelimishaji umma ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa taaluma hii kusimamiwa ipasavyo. Pia Bodi haina budi kusaidia waandishi wa habari kutumia teknolojia kwa manufaa ya taaluma yao bila kuvunja maadili.

Aliagiza Bodi hiyo ya kwanza kuteuliwa kuwa, haina budi kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi zao kwa usalama bila vitisho, unyanyasaji na vikwazo visivyo vya lazima, na kuongeza kuwa usalama wa waandishi wa habari ni msingi wa uhuru wa vyombo vya habari.