MCT kiungo muhimu sekta ya habari - Simbaya
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Kennedy Simbaya ( wa pili kulia walioketi) akiwa Msemaji mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Mobhare Matinyi (watatu kutoka kulia) na wageni wengine waalikwa waliohudhuria mkutano mkuu wa mwaka wa Muungano huo mjini Dodoma, Disemba 10, 2023.
Baraza la Habari Tanzania (MCT) ni kiungo muhimu sana kwa tasnia na sekta ya habari nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Bw. Kenneth Simbaya katika Mkutano Mkuu wa Muungano wa mwaka wa muungano huo uliofanyika Dodoma, Desemba 10, 2023.
Bw. Simbaya alisema ni muhimu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UTPC na wanatasnia ya habari nchini wakaelewa kuwa pamoja na kuwa kiungo muhimu sana kwa sekta ya habari, MCT pia ndiyo iliyofanya kazi kubwa kuisimamia na kuilea UTPC hasa katika uanzishwaji wa klabu za Waandishi wa habari na Sekretariati yake.
Akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa MCT Bw. Kajubi Mukajanga, Afisa Programu wa MCT – Bw. Tumbi Kiganja alisema kuwa Katibu Mtendaji ameomba udhuru kwa kutokuwepo katika mkutano huo kutokana na kuingiliana kwa ratiba, japo alitamani sana kuwepo hasa ukizingatia mahusiano yaliyopo kati ya MCT na UTPC.
Aidha, Tumbi alisema kuwa “Katibu ameniagiza niwashukuru UTPC kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa kutualika MCT kushiriki nanyi katika mkutano huu. MCT inaipongeza UTPC kwa dhati kwa kutimiza takwa la katiba yake kwa kukutanisha wanachama wake na kujadili mambo yanayohusu taasisi na tasnia kwa ujumla.
Kupitia Mkutano Mkuu huu Katibu Mtendaji wa MCT angependa kuwahakikishia wajumbe kuwa MCT inayo nia ya kudumisha ushirikiano wa kihistoria kati ya taasisi hizi mbili. Mahusiano haya yanatokana na dhima ya taasisi zetu ambayo ni kupigania maendeleo ya tasnia ya habari na wanahabari wenyewe hapa nchini.
Hivi sasa tunashirikiana katika masuala ya uchechemuzi unaolenga kupata sheria nzuri za habari na haki ya kujieleza. Tunashirikiana pia katika kupigania na kukuza usalama wa wanahabari, Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari – EJAT, na pia masuala ya mafunzo kwa wanahabari.
Katibu Mtendaji amesema anatarajia mashirikiano haya kuendelea na kupanuka zaidi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi aliyekuwa mgeni rasmi alisema kuwa Serikali siku zote imekuwa pamoja na Taasisi za kihabari na wanahabari kwa ujumla na kwamba wao (serikali) wanajua dhairi kuwa vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika Maendeleo ya taifa lolote.
“Vyombo vya habari ni muhimili muhimu sana katika Maendeleo ya taifa lolote hivyo Serikali ipo pamoja nanyi na tumekuwa tukufanya jitihada kukutana na wadau wa habari mara kwa mara kuangalia namna gani tunaweza kupunguza na kuondoa kabisa baadhi ya changamoto zinazo wakabili” alisema Matinyi.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC –Kenneth Simbaya akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu UTPC na Klabu za Waandishi wa habari, alizungumzia kuhusu maadhimisho ya siku ya Haki za Binadamu, pamoja na kuhitimisha kampeni ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Mkutano huo pia ulikwenda sambamba na uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa ulinzi na usalama kwa Waandishi wa habari ambao utakapokamilika utamwezesha mwandishi wa habari kutoa Taarifa mahala ambapo atajikuta yupo katika Mazingira hatarishi ya kiutendaji kazi.
Katika halfla ya kutoa tuzo kwa wanahabari iliyofanyika siku hiyo jioni kwenye ukumbi wa Makore katika jengo la PSSSF wanahabari sita wanawake watatu na wanaume watatu waliibuka washindi wa Tuzo za uadilifu kwa waandishi wa kike na kiume ambapo mshinid wa kwanza alipata tuzo, cheti na hundi y ash. Milioni 1.5, wa pili sh. milioni moja na watatu sh. 500,000. Washindi wa pili na watatu pamoja na zawadi ya fedha walipewa vyeti pia.
Tuzo ya Daudi Mwangosi haikupata mshindi safari hii.
Jaji kiongozi wa tuzo hizo, Chiku Lweno alisema walipitia kazi 52 zilizowasilishwa na wanahabari ambapo yeye na majaji wengine wawili Jesse Kwayu na Penina Robert walizipitia kwa umakini wa hali ya juu.