Tathmini ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) kuhusu hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini
Agosti 04, 2022
Kanzidata ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) imerekodi matukio 10 ya madhila ambayo waandishi wa habari wamekutana nayo katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Julai mwaka 2022.
Hii ni kwa mujibu wa kanzadata hiyo ambayo inapatikana kwenye www.pressviolations.or.tz
Madhila ambayo Baraza limeyarekodi kwenye kanzidata yake katika kipindi hicho ni matukio matatu ya vyombo vya habari kufungiwa, tukio moja la kunyanyaswa, matukio matatu ya kukamatwa, kunyimwa taarifa na matukio mawili ya waandishi kutishiwa.
Katika matukio hayo polisi wanaongoza kwa kuwa taasisi yenye migogoro na waandishi wa habari, ikifuatiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Matukio mengine ni ya waandishi wa habari kutishwa, yakitolewa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma tukio moja, na la watu wasiojulikana pia tukio moja.
Kipindi kama hiki mwaka jana kulikuwa na madhila 14 ya ukiukwaji wa haki za waandishi wa habari.
Madhila hayo kwa mwaka jana yalikuwa kufungiwa tukio moja, udhibiti hasi binafsi (self-censorship) (1), kukamatwa (4), kunyimwa taarifa (2), mauaji (1), vifaa kuharibiwa (1), na vitisho matukio manne.
Kwa mujibu wa kanzidata ya MCT, kipindi cha mwaka 2020 kanzidata hiyo ilirekodi matukio ya ukiukwaji wa haki za waandishi wa habari 43 wakati mwaka 2021, ilirekodi matukio 25.
Kwa jinsi hali ilivyo hivi sasa matukio hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka iliyopita.
Tumekuwa tukishuhudia mabadiliko kutoka kwa utawala ambao ulibana uhuru wa vyombo vya habari na wamiliki wa vyombo vya habari hadi kuvifuta mpaka utawala wenye kuanzisha mchakato wa kupitia sheria za vyombo vya habari ili kurekebisha sheria kandamizi kwa uhuru wa vyombo vya habari.
Kuthibitisha hilo, Februari 10, 2022, wakati akitoa leseni kwa magazeti manne yaliyokuwa yamefungiwa, Waziri Nape Nnauye aliweka wazi kuwa kufunguliwa kwa vyombo vya Mawio, Tanzania Daima, Mseto na MwanaHALISI yalikuwa ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa MCT, ishara ya kwanza kwamba mabadiliko yanakuja ilikuwa utayari wa mawaziri kufanya maongezi na wadau, ambapo wakati wa utawala uliopita Baraza lilihangaika bila mafanikio kwa muda wa miaka mitatu kupata nafasi ya kukutana na Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni bila mafanikio wala barua kujibiwa.
Lakini ndani ya utawala wa Rais Samia, katika kipindi cha miezi mitatu Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) ulikuwa umekutana na Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Waziri wa Katiba na Sheria ili kujadili mfumo wa kisheria unaoongoza vyombo vya habari. Baadae walikutana pia na waziri wa sasa wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Haya ni mabadiliko makubwa na ya kuungwa mkono.
Hapo awali tulishuhudia msururu wa sheria mpya zilizotungwa, wakati mwingine kwa hati ya dharura, na ambazo zilikandamiza uhuru wa vyombo vya habari, ambazo ni pamoja na Sheria ya Uhalifu wa Mtandaoni, 2015 na Kanuni zake za 2016, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, 2016, Kanuni za EPOCA (Maudhui ya Mtandaoni) 2018. Kitu ambacho kwa sasa hakionekani kujitokeza na sheria hizi hizi ziko katika mchakato kubadilishwa.
Kipindi kilichopita muda kama huu wa kati ya Januari mpaka Julai, wahariri wangekuwa wamepokea simu za kuonywa kuacha kuandika habari fulani, na simu hizo ni kutoka ndani na nje ya vyombo vyao vya habari.
Kutokana na hofu iliyokuwa imetanda katika tasnia ya habari, ilifikia hatua wamiliki wa vyombo vya habari wakawa wanaingilia uhuru wa uhariri kwa kuhofia leseni zao kufungiwa au kufutwa na mamlaka, kutokana na kurushwa au kuchapishwa kwa habari fulani.
Kubadilika kwa hali hiyo kunasababishwa na utayari wa kiongozi mkuu wa nchi ambaye ameonyesha kuithamini tasnia ya habari na kuwa tayari kufanya nayo kazi.
Matamshi ambayo yanatolewa na viongozi hasa wanaosimamia tasnia ya habari ni dalili tosha kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa tasnia ya habari tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo waandishi wa habari walionekana kama maadui wa serikali.
Kitu kikubwa cha kuzingatia ni kuhakikisha tunaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha sheria zote kandamizi zinafanyiwa marekebisho.
Tasnia ya habari inapaswa kukumbuka kuwa sheria kandamizi bado zimo vitabuni. Haki ya raia kujieleza na kupashana habari ni haki ya msingi na haipaswi kutegemea tu nia njema ya kiongozi aliyeko madarakani. Wakati tukimpongeza Rais kwa kuonyesha nia ya kuleta mabadiliko, hatupaswi kubweteka, tuendelee kusukuma mbele mchakato wa kubadilisha hizi sheria. Bila sheria kubadilika kicheko tulichonacho hivi sasa kunaweza kuwa cha muda mfupi.
Kajubi D. Mukajanga
Katibu Mtendaji