Katibu Mtendaji kufungua mafunzo kwa wahariri Zanzibar

 

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) anatarajia kufungua mafunzo ya siku tano ya wahariri na waandishi wa habari wa magazeti, radio TV na wale wa mtandaoni yatakayoanza Unguja Septemba 8, 2025, yakilenga kuimarisha uwezo wa kitaaluma na kisheria.

Mafunzo ya wahariri yatahusu namna ya kung’amua taarifa zisizo sahihi (misinformation), taarifa za uongo (disinformation) na hotuba za chuki au matamshi ya chuki (hate speech), zinazoweza kujitokeza kipindi cha uchaguzi mkuu.

Wakati mafunzo kwa waandishi wa habari yatahusu sheria za habari pamoja na changamoto zake, na baada ya hapo yatafuatiwa na cliniki za waandishi wa Habari mmoja mmoja Kwenda kuzungumza na mawakili kuhusu changamoto za kisheria wanazokutana nazo katika kazi zao.

Mafunzo haya, yatakayofanyika katika Ukumbi wa ZSSSF, Michenzani Mall, Zanzibar, zaidi ya wahariri 30 kutoka vyombo hivyo vya habari wakipatiwa fursa ya kujifunza mbinu za uhariri wa kisasa na kukabiliana na changamoto za habari potofu wakati wa uchaguzi.

Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa ni Pamoja na uadilifu na uwajibikaji wa wahariri wakati wa uchaguzi, changamoto za kimaadili katika kuripoti matukio ya uchaguzi, mfumo wa kisheria na maadili ya uandishi wa Habari.

Mada nyingine ni kuelewa wajibu wa kisheria na maadili ya kazi ya uhariri, mbinu za kuthibitisha taarifa na matumizi ya zana za kidijitali ili kuhakikisha usahihi na uhalisi wa taarifa kabla ya kuchapishwa.

Wahariri hao pia watapatiwa mbinu na mikakati ya vyumba vya habari kuelekea Uchaguzi 2025, ikijumuisha maandalizi, ujumuishaji wa timu, na mikakati ya uongozi wa habari wakati wa uchaguzi.

Wawezeshaji ni Saleh Yussuf Mnemo, Shadida Omar, Daniel Mwingira na Salim Salim, wataongoza mafunzo haya kwa kutumia mifano halisi, mbinu za vitendo na mapendekezo yanayoweza kutekelezeka mara moja katika vyumba vya habari.

Baada ya mafunzo ya wahariri, MCT itaendesha Kliniki za Kisheria kwa waandishi wa Habari, zitakazofanyikia katika ofisi za MCT Zanzibar, eneo la Mwanakwerekwe, ambapo waandishi 20 watashiriki.

Mada kuu zinazojadiliwa ni sheria zinazohusiana na kazi za waandishi wa habari, haki ya kupata taarifa na ushirikiano na serikali za mitaa, pamoja na msaada wa kisheria kwa waandishi wanaokabiliana na mashauri kazini. Wawezeshaji wa kliniki hizi watakuwa Shadida Omar, kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (THRDC), Hassan Kijogoo na Thabit Juma.

Mafunzo hayo yana lengo la kuhakikisha wahariri wanapata ujuzi wa kudhibiti taarifa potofu na hotuba za chuki, vyumba vya habari vina mikakati thabiti ya wakati wa kuandika Habari za uchaguzi, na waandishi wa habari wanapata msaada wa kisheria na uelewa wa haki zao kazini.

Matukio haya yanathibitisha dhamira ya MCT ya kuendeleza tasnia ya habari na kulinda uhuru wa uandishi, hususan katika kipindi cha uchaguzi.

Kwa kuandaa mafunzo haya Unguja, MCT itakuwa inapanua mpango wake wa kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa Habari, ambapo mpaka sasa imeshatoa mafunzo kama hayo Arusha, Mwanza na Dar es Salaam. Mwisho