TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Majaji kuamua kazi 1,135 Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania

Naibu Msajili wa Mahakama kuwaapisha kiapo cha uadilifu leo

 

Morogoro, Septemba 07 2024

Jopo la majaji saba wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2023 wanatarajia kuamua kazi bora zaidi za kiuandishi kati ya kazi 1,135 ambazo waandishi mbalimbali wa habari kote nchini wamewasilisha.

Mwamko wa waandishi wa habari kuwasilisha kazi za kihabari kuzishindanisha umekuwa ukiongezeka kwa miaka minne mfululizo. EJAT 2020 kazi zilikuwa 396, EJAT 2021 kazi zilikuwa 608, EJAT 2022 kazi zilikuwa 893 ambapo kazi za EJAT 2023 zimeongezeka hadi 1,135. Hii itakuwa ni mara ya 15 Baraza la Habari Tanzania na Washirika wake kuwatuza waandishi waliofanya vizuri katika kazi zao za kiuandishi tangu mwaka 2009.

Waandishi wa habari wa mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka huu wanaongoza kwa kuwasilisha kazi 290, wakifuatiwa na mkoa wa Arusha wenye kazi 81, Mwanza kazi 74, Iringa imeshika nafasi ya nne kwa kuwa na kazi 72, wakati mkoa wa Mtwara umeshika nafasi ya tano kwa kuwa na kazi 49.

Kwa upande wa Zanzibar, kazi zilizopokelewa ni kutoka Kaskazini Pemba (36) Pemba Kusini (43) na Mjini Magharibi (29).

Dirisha la kupokea kazi za waandishi wa habari lilifunguliwa tangu Novemba 15, mwaka jana na kufungwa Januari 31, mwaka huu. Kazi ya kuchambua na kutathmini ubora wa kazi za kihabari za mwaka 2023 inaanza leo baada ya Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Mhe. Fadhili Mbelwa kuwaapisha majaji.

Zoezi la kupitia kazi hizo linatarajiwa kuchukua kati ya siku saba hadi tisa, na linatarajia kufanyikia mkoani Morogoro katika moja ya hoteli zilizomo mkoani humo. Huu utakuwa ni mkoa wa pili zoezi hili kufanyikia mbali na Dar es Salaam. Mkoa mwingine ni Pwani.

Katika Tuzo za mwaka huu, MCT kwa kushirikiana na Mwananchi Communication Limited (MCL), watatoa Tuzo ya Zephania Ubwani kwa mara ya kwanza, ikiwa ni ishara ya kuenzi uandishi wa habari wa utaalam maalumu (specialization), ambao wakati wa uhai wake Zephania aliuishi na kuuhimiza.

Jopo la Majaji linaundwa na Mkumbwa Ally, Dkt. Egbert Mkoko, Eshe Muhiddin, Jeniffer Sumi, Halima Shariff, Halima Msellemu, na Absalom Kibanda.

Jopo limechaguliwa na wakuu wa taasisi za kihabari zinazounda Kamati ya Maandalizi ya EJAT 2023, kwa kuzingatia uadilifu, ujuzi na uzoefu wao katika uandishi wa habari, uwezo wa kuchambua na kutoa tathmini sahihi, uelewa wa mabadiliko ya kidigitali, uzoefu wa kimataifa au wa kijamii.

Aidha, jopo la majaji limezingatia uwiano wa kizazi kipya na cha zamani, waliopo kazini na waliostaafu, wabobezi wa maudhui mahsusi, usawa wa kijinsia, uwakilishi wa Zanzibar na Tanzania Bara na uwakilishi wa aina ya vyombo vya habari (magazeti, redio, runinga na mitandao).

Waandishi wa habari watakaoshinda watatambuliwa kwa ubora kwa kukidhi vigezo mbalimbali ambavyo ni pamoja na uwezo wa mwandishi wa habari kuchanganua, kutafsiri na kuripoti habari kwa usahihi na uadilifu, uandishi wa kina, uliojaa maarifa katika maudhui mahsusi.

Vigezo vingine ni uandishi wa kiufundi unaotumia lugha sahihi kwa mtindo unaovutia na kuelimisha, uthibitisho wa uwezo wa kuchunguza kwa kina, kuhoji vyanzo na kutathmini uhalali wa taarifa kabla ya kuripoti. Aidha ubora wa kazi za kihabari utazingatia ubunifu na uvumbuzi wenye namna mpya ya kuwasilisha habari au kuhusisha hadhira kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko.

Mbali na Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari, mchakato wa kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Maisha ya Mafanikio Katika Uandishi wa Habari (LAJA) 2024 umeshaanza. Tuzo hii humtambua mwandishi ambaye katika maisha yake ametoa mchango mkubwa katika kuiendeleza tasnia ya habari.

Baadhi ya magwiji waliopata Tuzo ya aina hii ni pamoja na Fili Karugahale Karashani, Mariam Mohamed Hamdan, Jenerali Twaha Ulimwengu, Hamza Mohamed Kassongo, Rose Haji Mwalimu, Ndimara Isaya Tegambwage, Dunstan Theodore Mhando.

Taasisi zinaounda Kamati ya Maandalizi ni Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Jukwaa la Wahariri (TEF), HakiElimu, Umoja wa Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Sikika na Twaweza.

Ernest S. Sungura

Katibu Mtendaji na

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya (EJAT) 2023