Katibu Mtendaji atembelea mali za Baraza

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura (mwenye truck suit) akionyeshwa mipaka ya shamba la MCT na mfanyakazi wa shamba hilo, Rajabu Ibrahimu Februari 8, 2024. Shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 13, lipo eneo la Zinga Wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Na mwandishi wetu

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura ametembelea mali za Baraza hilo vikiwemo viwanja 19 na mashamba yaliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Februari 8, 2024.

Ernest amefanya ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya kuzijua mali za Baraza hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni kiongozi mpya wa chombo hicho kikubwa nchini kinachosimamia vyombo vya habari.

Aidha, Ernest alifika kwenye kiwanja cha Baraza kilichopo Bagamoyo eneo la Kimalang’ombe na kufanya ukaguzi wa kiwanja hicho pamoja na miundombinu inayozunguka eneo hilo ili kuona namna gani ya kufanya uendelezaji kwa siku za usoni.

Kiongozi huyo wa Baraza pia alilitembelea shamba lenye ukubwa wa hekta 13, lilipo eneo la Zinga, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na kujionea shughuli zinazoendelea katika mali hizo za Baraza.

Ziara hii imekuja siku chache tangu akabidhiwe ofisi na mtangulizi wake Kajubi Mukajanga, Januari 16, 2024.

Pia Katibu Mtendaji huyo anatarajiwa kutembelea ofisi ya MCT Zanzibar ili kujionea shughuli zinazofanywa na ofisi hiyo pamoja na kukutana wafanyakazi na kuwaeleza mipango yake.

Wakati huo huo Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura Februari 8, 2024 alimtembelea mjumbe wa Bodi ya Wadhamini Mhe. Joseph Warioba nyumbani kwake, kama sehemu ya kujitambulisha na kumweleza mipango yake ya kuliendeleza Baraza.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa ziara za Katibu Mtendaji huyo wa kujitambulisha kwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), ambapo ameshamtembelea Profesa Geoffrey Mmari na Jaji Augusta Bubeshi.