TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Dar es Salaam
Baraza la Habari Tanzania (MCT) linasikitika kutangaza kifo cha rais wake na Mwenyekiti wa Bodi, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Juxon Isaac Mlay, aliyefariki dunia leo Mei 25, 2024 akiwa anapatiwa matibabu nchini India.
Jaji Mlay alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa rais wa MCT, Septemba 2020, akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Mhe. Jaji Thomas Mihayo. Alichaguliwa tena kwa muhula wa pili Septemba 2023 kuongoza Bodi ya MCT yenye wajumbe wanane.
Kabla ya kuchukua nafasi hiyo ya Urais wa MCT, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania, nafasi aliyoihudumu kwa kipindi cha miaka sita.
Jaji Mlay atakumbukwa kwa umakini wake wa kusimamia haki wakati wote wa usuluhishi uliotokana na ukiukaji wa maadili ya uandishi wa habari au kutozingatiwa kwa weledi wa kitaaluma. Aidha, kwa upande mwingine hakusita kuweka wazi kwa walalamikaji pale ambapo waandishi wa habari walipothibitisha kwa kujenga hoja za kuzingatia maadili na weledi wa kazi za kihabari.
Akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Jaji Mlay alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuzingatia maadili na weledi katika tasnia ya habari.
Hakusita kuvitembelea vyombo vya habari ambavyo vilikuwa na changamoto mbali mbali zikiwemo za kimaadili, na kutoa ushauri wa namna bora ya kuondokana na changamoto hizo.
Katika awamu yake ya kwanza ya uongozi akiwa Mwenyekiti na Rais wa MCT ameliongoza Baraza kwa umahiri mkubwa na kulipitisha katika michakato ya uendelevu wa kitaasisi. Aidha, Jaji Mlay alisimamia kikamilifu mchakato wa kumpata mrithi wa nafasi ya Katibu Mtendaji mpya wa MCT, Ndugu Ernest Sungura aliyechukua nafasi ya Ndugu Kajubi Mukajanga mapema Januari 2024.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kufika Dar es Salaam, Mei 28, 2024 saa 3:20 asubuhi kwa Shirika la Ndege la Air Tanzania na utaagwa Jumatano Mei 29, 2024 katika kanisa la Azania Front kuanzia saa 4 asubuhi. Mazishi yanatarajiwa kufanyika Ijumaa, Mei 31, 2024, Himo wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Jaji Mlay ni Jaji mwenye hadhi ya juu, aliyewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ambaye kabla ya hapo alihudumu kama mwandishi wa sheria za Bunge na Mwendesha mashtaka.
Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mjumbe wa Bodi ya MCT mwaka 2014 ambapo aliongoza Kamati ya Maadili ya Baraza kutoka 2014 hadi 2017, na alichaguliwa tena tarehe 29 Septemba 2017 kushika wadhifa huo. Aliendelea kuongoza Kamati ya Maadili, huku pia akiwa mjumbe wa Kamati ya Hesabu za fedha.
Mwaka 1977 hadi 1981 alihudumu kama Msaidizi wa Mwandishi wa Sheria za Bunge, ambapo baadaye mwaka 1981 hadi 1986, alihamishiwa kwenye Kikosi cha Kupambana na Rushwa (sasa PCCB) na kuwa mkuu wa Kitengo cha Sheria na Mashtaka. Mwaka 1987 hadi 1989, alipandishwa cheo na kuwa Msaidizi Mwandamizi wa Mwandishi wa Sheria za Bunge.
Mhe. Jaji Mlay kati ya mwaka 1989 hadi 1991 alihamishiwa kwenye Sekretarieti ya Bunge na kuteuliwa kuwa Karani Mwandamizi wa Bunge. Mwaka 1991 hadi 1993, aliteuliwa kuwa Naibu Mwandishi Mkuu wa Sheria za Bunge.
Kati ya mwaka 1993 na 1997, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa kwanza wa Masuala ya Katiba katika Wizara ya Sheria na Masuala ya Katiba, ambapo mwaka 1997 hadi 2000, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (D.P.P).
Jaji Mlay kutokana na umahiri wake katika utendaji kazi mwaka 2000 hadi 2009 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, nafasi aliyokaa kwa miaka tisa na kisha kustaafu mwaka 2009.
Baraza la Habari Tanzania (MCT) limempoteza kiongozi mahiri, muadilifu na makini. Mungu awape subira na ustahimilivu mke wake, watoto na ndugu wote walioguswa na taarifa nzito za msiba wa Rais wa MCT.
Bwana Mungu ametoa na Bwana Mungu ametwaa, Jina la Bwana Mungu lihimidiwe.
Imetolewa na:
Ernest S. Sungura
Katibu Mtendaji
Mei 25, 2024