MCT Yamuenzi Jaji Mlay

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeendelea kumuenzi aliyekuwa rais wa Baraza hilo, Jaji Juxon Mlay, kutokana na mchango wake kwa MCT na tasnia ya habari. Jaji Mlay alifariki dunia Mei 2024, nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

 Akizungumza nyumbani kwa familia ya Jaji Mlay, mwishoni mwa wiki, rais wa Baraza la Habari Tanzania, Jaji Bernard Luanda, amesema wakati wa uhai wake Jaji Mlay, alikuwa ni kiongozi aliyenyooka katika utendaji kazi wake na hakupenda uonevu. Amesema Jaji Mlay anastahili kukumbukwa na kuenziwa kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka kwa MCT na kwa tasnia ya habari nchini.

 Jaji Luanda ameyasema hayo alipoongoza ujumbe wa watu sita kutoka MCT ulioitembelea familia ya kiongozi huyo, kwa lengo la kuijulia hali. Uongozi wa MCT ulitumia muda huo kushauriana na familia namna ya kuendelea kumuenzi Jaji mstaafu marehemu Mlay.

 Wajumbe wengine katika ziara hiyo ni Sophia Komba, ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya MCT, Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura na wafanyakazi wanne wa Baraza hilo, Mwanzo Millinga, Bertha Christopher, Esther Mkanza na Athumani Mbegu.

 Mjane wa marehemu Jaji Mlay, Florah Mlay, amesema wakati wa uhai wake Jaji Mlay alikuwa mwadilifu nyumbani na kazini kwake. Ameongeza kuwa amefurahishwa na ziara ya ujumbe huo kumtembelea.

 Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu Mtendaji wa MCT, amesisitiza kuwa Baraza litaendelea kuwa karibu na familia hiyo kutokana na kuthamini mchango wa Jaji Mlay kwa MCT na kwa tasnia ya habari.

 Wakati wa uhai wake Jaji Mlay aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania, nafasi aliyoishika kwa miaka sita mfululizo na baada ya hapo akawa rais wa MCT. Huyu ni kiongozi wa kwanza wa juu wa  MCT kufariki akiwa madarakani. Alikuwa rais wa tano baada ya Pof. Geoffrey Mmari, Prof Issa Shivji, Jaji Robert Kisanga, na Jaji Thomas Mihayo.