Taarifa kwa vyombo vya habari
Taarifa kwa vyombo vya habari
Desemba 20, 2024
Dar es Salaam: Baraza la Habari Tanzania (MCT), linawatarifu waandishi wa habari kuwa kwa mwaka huu, Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT), utafanyika tofauti na ilivyozoeleka.
Hii ni pamoja na muundo wake wa kategoria, namna ya kupata washindi na muda wa kuwasilisha kazi kwa ajili ya mashindano, vyote vitakuwa tofauti na miaka iliyopita.
Dirisha la kupokea kazi za waandishi wa habari kwa ajili ya kushindanishwa litafunguliwa Februari 28, 2025, ambapo waandishi wa habari watatakiwa kuanza kuleta kazi zao zilizochapishwa au kurushwa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 31, 2024 na Januari hadi Oktoba kwa mwaka 2025.
Kutokana na utaratibu huo mpya, shughuli ya utoaji Tuzo inatarajiwa kufanyika Desemba 2025, ili kutoa nafasi kwa waandishi wa habari kujiandaa kwa kuandika habari zenye tija, zilizofanyiwa utafiti wa kina na zenye kuibua suluhisho la changamoto za wananchi.
Kwa upande wa makundi ya kushindanisha utaratibu utakuwa kama ifuatavyo:-
- Mwandishi ataruhusiwa kuleta kazi zake kwa kushauriana na mhariri wa chombo anachofanyia kazi kama kawaida. (magazeti, TV, radio na vyombo vya habari za mtandaoni);
- Wananchi kupigia kura chombo cha habari ambacho kinatoa habari zenye suluhisho kwa changamoto za wananchi (magazeti, TV, radio na vyombo vya mtandaoni)
- Jopo maalum la watalaam wa habari kuchagua habari, kipindi, au vipindi vilivyoandaliwa kwa kufuata maadili ya uandishi wa habari na weledi mkubwa. (magazeti, TV, radio na vyombo vya mtandaoni).
- Tuzo ya Maisha ya Mafanikio Katika Tasnia ya Habari: Tuzo hii mwandishi nguli haleti kazi yoyote kwa jopo la majaji, isipokuwa unaangaliwa mchango wake kwa sekta ya habari wakati wa uandishi wake.
Kazi zitakazohusishwa katika utaratibu huu mpya ni zile zilizochapishwa au kurushwa katika kipindi cha mwaka 2024 na 2025.
Utaratibu huu mpya una malengo yafuatayo:-
- Kutambua kazi zilizowasilishwa na zile ambazo hazikuwasilishwa kwenye mashindano; na
- Kuzipeleka tuzo hizi kwa wananchi kwa kuwashirikisha kupiga kura kuchagua kipindi bora, mtangazaji bora, taarifa ya habari bora na chombo bora cha habari.
Makundi yote hapo juu yatakuwa na vigezo ambavyo vitatoa mwongozo wa ni sifa zipi zinafanya habari fulani au kipindi fulani, au chombo fulani cha habari kuwa na sifa za kushinda.
Baraza linaamini kwa kufanya maboresho hayo EJAT itaendelea kuwa na mvuto zaidi na kuwa kipimo cha juu kabisa katika nchi cha kupima umahiri wa uandishi wa habari.
Pamoja na hayo nichukue fursa hii, hasa tunapoelekea kusherehekea Sikukuu za Krismas na Mwaka mpya 2025, kuwatakia heri na fanaka tele wanachama wote wa Baraza, waandishi wa habari, washirika wa maendeleo na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, sikukuu njema ya Krismas na mwaka mpya wenye heri na mafanikio tele.
Mwaka mpya wa 2025 uwe mwaka wa kushirikiana, kuzungumza na kujadili changamoto na mafanikio ya sekta ya habari.
Ernest Sungura
Katibu Mtendaji