Lowassa, rafiki wa dhati wa vyombo vya habari

Hayati Edward Ngoyai Lowassa.

 

Na Kajubi Mukajanga

Mara nyingi nikifikiria urafiki kati ya vyombo vya habari na wanasiasa huwa nakumbuka mchoro wa picha za mafuta ambao ulikuwa mashahuri nilipokuwa mdogo. Mchoro huu ni wa simba akiwa na swala wameketi pamoja kama marafiki wanaopiga soga. Chini ya picha hii yalikuwapo maandishi: “Urafiki wa Mashaka.”

Hata hivyo, kuna mwanasiasa mmoja ambaye nilimfahamu kama rafiki wa dhati wa vyombo vya habari: Edward Ngoyai Lowassa.

Nilimfahamu Lowassa miaka ya mwanzo ya 1990 akiwa mbunge na waziri, nami nikiwa mhariri wa gazeti la Wakati ni Huu. Lakini ushahidi wa kwanza muhimu niliouona katika mahusiano yake na vyombo vya habari ulikuwa mwaka 1997. Yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kabisa kupeleka shauri lake katika Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa ajili ya utatuzi na usuluhishi.

Tukio hili ni muhimu katika historia ya vyombo vya habari Tanzania maana MCT ndio ilikuwa imeanza kazi baada ya kupata usajili rasmi tarehe 22 Mei, 1997 kufuatia kuundwa na wanahabari 30 Juni, 1995.

Kesi ya Lowassa dhidi ya gazeti la Heko ilikuwa ni mtihani muhimu kwa asasi hiyo changa iliyopigia upatu utaratibu wa vyombo vya habari kujisimamia vyenyewe (self-regulation).

Tarehe 27 Agosti, 1997 gazeti la Heko lilichapisha habari kubwa ukurasa wa kwanza iliyodai kuwa Edward Lowassa na “vigogo wengine” walikuwa wamebainika kuwa walitajwa katika ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Kero ya Rushwa, maarufu kama Tume ya Warioba ya Rushwa.

Itakumbukwa kuwa baada ya kuingia madarakani, Rais Benjamin Mkapa aliunda tume iliyoongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Warioba kuchunguza mianya ya rushwa na kutoa mapandekezo.

Katika taarifa ya Heko iliyokuwa na kichwa cha habari: Tume ya Kero ya Rushwa: Baadhi ya viongozi, vigogo, ambao watafikishwa mahakamani wafahamika: Yumo … Mh. Lowassa … na wengineo, gazeti lilidai kuwa katika ziara ya Mkoani Ruvuma Rais Mkapa alikuwa ameahidi kuwa watu wote waliotajwa katika ripoti ya Warioba wangefikishwa mahakamani na kwamba gazeti lilikuwa limebaini kuwa mmoja wao ni Lowassa.

Katika malalamiko yake mbele ya Kamati ya Maadili ya MCT, Lowassa alisema habari hiyo ilikuwa ya uongo, ilimchafua, na pamoja na yeye kuwasiliana na gazeti, lakini lilikuwa limekataa kuchukua hatua za kumsafisha.

Lowassa alidai kuwa aliamini kuwa gazeti lilikuwa na “ajenda ya siri” dhidi yake kwa kuwa lilikuwa na mtindo wa kuandika habari za kashfa dhidi yake ikiwamo ile iliyodai kuwa alikuwa ametumia shilingi milioni 50 kwenye kampeni yake ya mwaka 1995.

Alisema licha ya Profesa Rwekaza Mukandala wa Kamati ya Kufuatilia Uchaguzi ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambaye gazeti lilimtaja kama chanzo chao kukanusha habari hiyo, bado gazeti halikufanya marekebisho wala kuomba radhi kwa taarifa hiyo ya uzushi.

Pamoja na kwamba Lowassa angeweza kwenda mahakamani ambapo ikiwa angeshinda angeweza kupata fidia kubwa ya pesa, au kulalamika kwa waziri wa Habari – mkubwa mwenzie – ili achukue hatua kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, Lowassa aliamua kwenda MCT, taasisi ambayo ilikuwa haijawahi kusikiliza shauri lolote, na ambayo ilikuwa imeundwa na wanahabari hao hao anaowalalamikia.

Ni imani hii katika mfumo huu mpya, wa wanhabari kujisimamia wenyewe, ambayo inaifanya kesi hii kuwa ya kihistoria.

Kamati ya Maadili ya MCT ambayo ilikuwa na jukumu la kusikiliza malalamiko ilikuwa na wajumbe saba: wanasheria wawili na wanahabari watano. Iliongozwa na Jaji Joseph Warioba, makamu wake akiwa Dk. Sengondo Mvungi.

Wajumbe wengine, wanahabari, walikuwa Lawrence Kilimwiko, Salim Said Salim, Jenerali Ulimwengu, Marie Shaba, na Danford Mpumilwa.

Kwa kuwa mwenyekiti wa Kamati alikuwa mtu yule yule aliyeongoza tume inayosemekana ilimtaja Lowassa kama mmoja wa wala rushwa, Jaji Warioba alijiondoa katika kusikiliza shauri hilo, akimwachia makamu wake Dk. Mvungi. Katibu Mtendaji wa Baraza alikuwa Anthony Ngaiza.

Shauri lilisikilizwa tarehe 23 Septemba, 1997. Uamuzi uliofikiwa na Kamati ulikuwa kwamba gazeti lilikiuka vipengele kadhaa vya Kanuni za Maadili za Wanataaluma ya Habari.

Heko iliamriwa kuomba radhi, na kulipa fidia ya usumbufu ya shilingi milioni moja, ambazo Lowassa alitaka zipelekwe kwa vituo vya watoto yatima. Mchapishaji wa gazeti hilo, Ben Mtobwa, alikubali na kutekeleza maamuzi hayo, na shauri likafungwa.

Shauri hili liliipa MCT umashuhuri na uhalali mbele ya wadau wa habari, na muhimu wananchi, ambao walianza kupeleka malalamiko yao pale walipochukizwa au kuumizwa na mwenendo wa vyombo vya habari. Watu wakajua kwamba badala ya kwenda mahakamani kutumia fedha na muda mwingi, kulikuwa na chombo ambacho kingeweza kusikiliza mashauri na kuyatolea maamizi au kuyasuluhisha bila gharama kubwa, na kwa muda mfupi.

Lakini hilo halikuwa tukio pekee.

Lowassa alipeleka shauri jingine MCT kuhusiana na taarifa sita zilizochapishwa na gazeti la Dira ya Mtanzania kati ya Oktoba 2011 na Novemba 2011, zikimshutumu na kumtuhumu Lowassa kwa mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukihujumu chama cha CCM mkoani Arusha, kumhujumu Rais Jakaya Kikwete, na masuala ya uadilifu.

Kikao cha kusikiliza shauri hilo kilifanyika tarehe 20 Septemba, 2012 chini ya mwenyekiti wake Jaji Thomas Mihayo, lakini gazeti halikutokea, wala kutekeleza maamuzi ya Kamati.

Pamoja na kwamba Lowassa angeweza kupeleka mashtaka mahakamani baada ya ukaidi wa gazeti, hakufanya hivyo, akisema malalamiko yake yalikuwa yamesikilizwa na chombo cha tasnia na kutolewa maamuzi na kwake hiyo ilitosha.

Hata hivyo, baadae Kamati ya Maadili ya MCT ilipotembelea ofisi za Msama Promotion na Dira Company Limited, wamiliki na wachapishaji wa gazeti hilo, Mkurugenzi Bw. Msama alikiri makosa na kuonyesha mshtuko kwa jinsi mambo yalivyokuwa yakiendelea katika ofisi yake.

Badala ya kuchukua njia za kuvipatiliza vyombo vya habari kwa mkondo wa mahakama, Lowassa ni mwanasiasa ambaye alichagua njia ya usuluhishi pale alipoona ametendewa visivyo.

Urafiki usio wa mashaka wa Lowassa kwa vyombo vya habari ulijidhihirisha pia kwa matendo mengine.

Wakati kikundi cha waandishi kilipoanzisha kampuni ya Habari Corporation iliyochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai na mengineyo, moja ya changamoto kiliyopata ilikuwa ni ofisi.

Lowassa aliahidi kuwasaidia, na mara chama cha ukombozi wa Afrika Kusini cha Pan Africanist Congress of Azania (PAC) kilipohama kutoka ofisi zake zilizokuwa mtaa wa Mkwepu katikati ya jiji la Dar es Salaam, Lowassa, akiwa Waziri wa Ardhi, alihakikisha Habari Corporation inapata ofisi hapo.

Hata katika safari zake za kikazi, alihakikisha wanahabari wanakuwapo. Japo kama mwanasiasa yeyote makini nae alitaka kutangazwa, lakini pia alielewa umuhimu wa wananchi kujua serikali yao inafanya nini kupitia vyombo vya habari.

Nilipokuwa mhariri wa Wakati Ni Huu miaka ya mwanzoni ya 1990 na yeye akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu tulichapisha habari kadhaa “nyeti” zilizogusa maslahi ya wafanyakazi wa usalama wa taifa.

Tulishafahamiana na nilijua habari hizo zilikuwa zikimsumbua. Lakini tulipokutana, alichonambia tu ni: “Kajubi, unapata wapi habari hizo zisizokanushika?”

Mwaka 1995 nchi ilipokuwa katika joto kubwa la uchaguzi wa vyama vingi baada ya miongo kadhaa, nilifanya mahojiano maalum na aliyekuwa mkuu wa majeshi, Jenerali Robert Mboma.

Msingi wa mada ya mahojiano yetu ulikuwa nafasi ya jeshi katika mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo, mazungumzo yetu baadae yalikwenda katika mambo mbalimbali, na baadhi yakagusa mambo ya watu wakubwa jeshini.

Gazeti lilipotoka na habari hizo ikawa “kizaazaa”! Ni wazi, kuna watu wenye nguvu ambao hawakufurahia habari zile. Zilikuwa taarifa mbili au tatu, zote ukurasa wa kwanza.

Ndipo msaidizi wa Lowassa, Saidi Nguba, alipokuja ofisini Sinza na kunipa wito wa Lowassa, akitaka kuzungumza nami kesho yake asubuhi.

Niliitikia wito.

Kesho yake, Jumamosi, nikaenda ofisini kwa Lowassa akiwa Waziri wa Ardhi. Alikuwa mcheshi sana, na hatimae akaleta suala la taarifa ile iliyohusu masuala ya matumizi ya wakubwa, ambayo chanzo nilikuwa nimekihifadhi.

Yeye hakugusia habari kuu, ambayo nilishapata lawama kutoka kwa wakubwa wengine kwamba mahojiano yangu yalikuwa yamewajenga wapinzani. Jenerali alikuwa amezungumza kwa kirefu na akahitimisha kwamba jeshi litaheshimu maamuzi ya wananchi bila kujali wamechagua chama au mgombea gani.

Lowassa akanifahamisha kuwa baadhi ya wakubwa jeshini walikuwa wamechukizwa sana na taarifa hiyo kuhusu matumizi. “Shida ni kwamba haikanushiki,”akanambia, na kuongeza,, “Na inaonekana chanzo chako ni cha juu.”

Nikakaa kimya.

“Kwa hiyo ni chanzo cha juu mno,” akadadisi.

“Unajua siwezi kuzungumzia source (chazo) wangu,” nikamjibu.

“Basi nitayamaliza. Watu wanasema mambo ya kutisha. Nashauri kuwa hiyo stori uliyoandika inatosha. Usijihatarishe.”

Tukaendelea na maongezi mengine, lakini nilikuwa na mshtuko, na nikapata funzo. Nilikuwa mhariri, lakini uzoefu wangu haukuwa mkubwa sana. Nikajifunza kuwa kila chanzo cha habari kina sababu ya kukupatia taarifa kinazokupa. Ni juu ya mhariri kufanya maamuzi ya kitu gani atumie.

Lowassa alipenda waandishi na vyombo vya habari. Alipoteuliwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 1990 aliamua msaidizi wake awe mwandishi wa habari, akamchukua Saidi Nguba kutoka Uhuru na Mzalendo.

Hata alipohamia Wizara ya Ardhi alihama nae, na baadae alipokuwa Waziri Mkuu alimchukua katika nafasi ya Mwandishi wa Waziri Mkuu.

Nguba anaarifu kuwa Lowassa alikuwa source mzuri wa wahariri wengi. Aliwapa tip na hata scoop. Aliwapenda na kuwathamini wanahabari, na kila wakati alikuwa tayari kuongea nao na kuwasaidia.

Mungu ailaze pema roho ya marehemu Edward Ngoyai Lowassa.

 

https://lukwangule.blogspot.com/2012/09/lowassa-aipeleka-dira-ya-mtanzania.html

 

https://lukemusicfactory.blogspot.com/2012/09/dira-ya-mtanzania-laamriwa-kumuomba.html