Serikali yahimizwa kuifanyia marekebisho Sera ya Habari

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura (kushoto) akizungumzia shughuli zinazofanywa na MCT katika kituo cha redio cha Metro kilichopo jijini Mwanza. Wengine katika picha hiyo ni wasaidizi wa Katibu Mtendaji huyo, Said Hassan na Elizabeth Munisi.

 

Februari 13, 2025: Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeikumbusha Serikali kuharakisha mchakato wa kuifanyia marekebisho Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003, ambayo imepitwa na wakati kwa sasa.

Sera hiyo ambayo ilitakiwa itoe dira ya utungwaji wa sheria zinazosimamia Sekta ya Habari, kama Huduma za Habari, 2016, Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa, 2016, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, 2015, Sheria ya Kieletroniki na Mawasiliano ya Posta, 2010, lakini sheria zimekuwa zikibadilishwa na kwendana na wakati, huku Sera ikibaki kuwa ya zamani.

Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura aliyasema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Redio Duniani, ambayo huadhimishwa kila Febrauri 13, ya kila mwaka.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Redio kwa Mabadiliko ya Tabia Nchi” ikiwa na lengo la kuhamasisha mijadala katika redio iliyojikita katika kutoa elimu, kuhamasisha mabadiliko endelevu na kuzishirikisha jamii katika majadiliano yanayoangazia mabadiliko ya tabia nchi.

“Katika kuadhimisha siku ya redio duniani, MCT inatoa wito kwa Serikali kukamilisha maboresho ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 ambayo iliuanzisha Oktoba mwaka 2023 kwa kuita wadau kupeleka maoni yao ambapo MCT iliwasilisha maoni yake,” alisema katika taarifa hiyo.

Alisema sekta ya redio  inakumbwa na changamoto za kiuchumi na za kisheria ambazo zinakwamisha maendeleo na ukuaji wa redio nchini.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, katika Kongamano la Kitaifa la Maendeleo ya Sekta ya Habari lililofanyika Juni 2024, MCT ilisisitiza umuhimu wa kukamilishwa kwa maboresho ya Sera hiyo.

Baadhi ya maboresho yaliyowasilishwa serikalini ni pamoja na kipengele namba 2.3.2 ambacho kinazungumzia umiliki wa vyombo vya habari, wakitaka Sera ielekeze serikali kuhakikisha inatunga sheria itakayowezesha wawekezaji kutoka nje ya nchi usiwe na ukomo wa umiliki wa hisa, ambapo kwa sasa mwekezaji anatakiwa kumiliki asilimia 49.

Pia wadau wanapendekeza kuwa Sera ielekeze mwekezaji wa ndani anapoingia ubia na mwekezaji wa nje hisa zake zisipungue asilimia 25. Tafadhali bonyeza hapa ili upate mapendekezo ya MCT kwa Serikali.

Akizungumza na wadau wa habari Disemba 18, 2024 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof Palamagamba Kabudi alitaja marekebisho ya Sera hiyo kama moja ya vipaumbele vyake na kwamba atasimamia mchakato wa uboreshaji wa Sera hiyo.

MCT inaamini kwamba kukamilika kwa uboreshaji wa Sera hiyo kutaharakisha marekebisho ya sheria na kanuni nyingine ambazo kwa sasa zinaathiri uendeshaji wa sekta ya habari na utangazaji.