NI EJAT YA AINA YAKE

Na Paul Mallimbo

Ilikuwa ni Jumamosi ya Septemba 28, 2024 iliyojaa furaha na shauku kwa tasnia ya habari nchini kutaka kujua washindi wa EJAT 2023, ambapo jumla ya wateule 72 wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2023, waliingia kwa shauku kubwa ukumbini kutaka kujua nani ataibuka kidedea katika Tuzo hizo.

Ilipofika saa 10:39 jioni mgeni rasmi wa Tuzo hizo Naibu Spika, Mhe. Mussa Azzan Zungu, ambaye alimwakilisha Mhe. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliingia ukumbini Aga Khan Diamond Jubilee.

Shughuli hiyo ilianza kwa ukaribisho kutoka kwa mwenyeji wa Tuzo hizo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania, Ernest Sungura, ambaye pamoja na kuukaribisha umma uliokuwepo ukumbini pia aliukaribisha umma uliokuwa ukifuatilia Tuzo hizo moja kwa moja kupitia runinga za Channel Ten, TBC1 na UTV.

Hii ikiwa ni mara ya 15 tuzo hizo zikifanyika, ambapo mara 14 zikiwa chini ya Katibu Mtendaji, Kajubi Mukajanga na mara moja chini ya Katibu Mtendaji wa sasa Ernest Sungura. Ikumbukwe kuwa Katibu Mtendaji pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT.

Burudani ya ngoma kutoka kikundi cha Dar Creators ilitoa burudani murua iliyokonga nyoyo za wageni waalikwa akiwemo mgeni rasmi na meza kuu yote.

Katika Tuzo hizo pia Rais mpya wa Baraza la Habari Tanzania, Jaji Bernard Luanda alitambulishwa mbele ya umati wa watu uliohudhuria Tuzo hizo pamoja na wananchi wengine waliozishuhudia wakiwa majumbani kwao.

Ukumbi huo ambao ulifunikwa kwa rangi ya bluu, shamsham, ngoma, mbwembwe kutoka waandishi wa habari waliokuwa wanashangilia wenzao kutoka chombo chao wakipokea tuzo mbalimbali, ulimsikia mgeni rasmi akiwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuhakikisha nchi inakuwa salama.

Mhe. Zungu alilipongeza Baraza na washirika wake kwa maandalizi ya Tuzo hizo, akisema, “Sote tunafahamu umuhimu wa vyombo vya habari katika kujenga taifa lenye mshikamano wa dhati.”

Alimnukuu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusema, “Tumieni kalamu zenu na vyombo vya habari kuilinda nchi. Ni dhahiri kwamba kalamu ina nguvu kuliko upanga katika kulinda amani ya nchi yetu ambayo ni tunu ya taifa letu,”

Kilele hicho cha Tuzo kilisindikizwa na mandhari nzuri iliyokuwepo ukumbini hapo ambapo mabango yaliyojaa nembo za washirika na wafadhili wa EJAT 2023 yalitapakaa kila kona ya ukumbi. Ilikuwa siku ya furaha na nderemo tele.

Tuzo hizo mbali na kuwakutanisha wateule wa EJAT 2023, pia waandishi wa habari wakongwe, kama Hamzo Kasongo, Mshindi wa Tuzo za Maisha katika Uandishi wa Habari, Bakari Machumu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications (MCL) mstaafu, Hamisi Mzee, Abdi Sultani, Derek Murusuri, Edda Sanga, Dkt. Samwilu Mwaffisi na wengine wengi walihudhuria Tuzo.

Washindi wa Jumla kwa miaka tofauti Neville Meena (2012), Hilda Phoya (2019) na Sanula Athanas, (2022) nao walikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria kilele cha Tuzo hizo.

Jopo la majaji wa EJAT ambao nao walihudhuria sherehe hizo wakiwa wamependeza sana, waliongozwa na Jaji Kiongozi wao Halima Shariff, na Katibu wa Jopo, Dkt. Egbert Mkoko. Wengine walikuwa ni Eshe Muhiddin, Mkumbwa Ally, Halima Msellem, Jennifer Sumi na Absalom Kibanda pia walikuwepo kushuhudia matunda ya kazi yao.

Jopo hilo la majaji lilifanya kazi kwa takribani siku 10, huku likipitia kazi 1,135 zilizowasilishwa katika kinyang’anyiro hicho ambacho kilitoa wateule 72 kutoka pande zote za Tanzania.

Akitoa hotuba yake Jaji Kiongozi Halima Shariff alisema kuwa uandishi wa habari umeendelea kukua japo changamoto pia hazikukosekana. Alisema kuwa walipokea habari ambazo hazikuwa na kishindo na zipo zilizokosa utafiti wa kina kitu ambacho pia ni changamoto kwa wahariri wetu.

Kilele hicho kilichokuwa na matukio mbali mbali kutoka kwa waandsihi wa habari na wacheza ngoma, pia kilishuhudia mwakilishi wa mgeni rasmi, Naibu Spika Mhe. Zungu akimtaja Mukrim Mohammed Khamis, kuwa mshindi wa jumla wa Tuzo za Umahiri wa Uandshi wa Habari Tanzania kwa mwaka 2023.

Kijana mtanashati aliyevalia bleza krimu, shati jeupe na suaruali nyeusi, alilishukuru Baraza kwa kuhakikisha Tuzo hizo zinafanyika kila mwaka bila kukosa.

Mukrim ni kijana mwenye ngozi ng’avu, ni mfupi anayeandikia vyombo vya habari vya mtandaoni. Alisema yeye anapenda kuandika habari za kina na zenye utafiti wa kutosha.

Anasema kuna nyakati hulazimika kurudi field ili kutafuta habari zenye kishindo kwa jamii, “Mimi habari za kualikwa kwenye mawizara hautanikuta hata mara moja. Mimi nafanya stori zenye kuibua changamoto za wananchi ili ziweze kufanyiwa kazi na watunga sera.”

Anajinadi kuwa mipango yake ni kuwa na kituo ambacho kitawasaidia waandishi wa habari kule Zanzibar kupata mafunzo ya namna ya kuandika habari za mtandaoni zenye kufuata maadili na tija kwa jamii.

Kijana Mukrim anasema ana mahaba na habari zinazohusu mazingira, na habari zilizompa ushindi wa jumla zilihusu Jitihada za kukuza uchumi wa buluu Zanzibar na Mazingira yanavyoathiri uchumi wa buluu Zanzibar.

Kabla ya kutangazwa kuwa mshindi wa jumla alishika nafasi ya kwanza katika kundi la Habari za Biashara, Uchumi na Fedha kwa kipengele cha vyombo vya habari vya mtandaoni na kwenye kundi la Uandishi wa Habari za Utunzaji wa Mazingira na vyanzo vya Maji.

Tuzo hizi pia kwa mara ya kwanza zimekuja na jarida lijulikanalo kama Jarida la TUZO lenye lengo la kuibua uandishi wa kina kwenye kulenga habari zenye visindo. Lakini pia Jarida hilo linalenga kuwaibua waandishi wa habari wakongwe ambao wameifanyia tasnia kazi iliyotuka ikiwa ni pamoja na kutoa mchango mkubwa katika tasnia.

Jarida la TUZO linalenga pia kutoa maelezo kuhusu washindi waliochukua, kuwajua kiundani wao na maisha yao pamoja na changamoto mbali mbali ambazo wamekutana nazo.

Jarida hilo lilizinduliwa Septemba 28, 2024 katika kilele cha Tuzo hizo, ambapo linatarajiwa kusambazwa kwa kila mshiriki aliyehudhuria Tuzo hizo ili kujionea kiwango cha juu cha ubunifu ulioonyeshwa na waandishi wa habari mahiri katika kuandika habari zenye utafiti, zenye mtindo mwanana na zenye kishindo.

Makundi yaliyoshindaniwa kwa 2023 ni pamoja na Tuzo ya Uandishi wa Habari za, Biashara, Uchumi na Fedha; Tuzo ya Uandishi wa Habari za Utamaduni na Michezo;

Tuzo ya Uandishi wa Habari za Kilimo na Biashara ya Kilimo;Tuzo ya Uandishi wa Habari za Elimu; Tuzo ya Uandishi wa Habari za Utalii na Uhifadhi; na Tuzo ya Uandishi wa Habari za Uchunguzi.

Nyingine ni Tuzo za Uandishi wa Habari za Data; Tuzo za Uandishi wa Habari za Haki za Binadamu na Utawala Bora; Tuzo ya Uandishi wa Habari za Jinsia na Watoto; Tuzo za Uandishi wa Habari za Walemavu; Tuzo za Uandishi wa Habari za Afya; Tuzo za Uandishi wa Habari za Ushirika; na Tuzo za Uandishi wa Habari za Kodi, Tozo na Mapato.

Palikuwa pia na Habari za Uandishi wa Habari za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii; Tuzo ya Uandishi wa Habari za Utunzaji wa Mazingira na vyanzo vya Maji; Tuzo ya Uandishi wa Habari za Afya ya Uzazi; Tuzo ya Uandishi wa Habari za Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto; Tuzo ya Uandishi wa Habari za Mafuta, Gesi na Uchimbaji Madini na Kundi la Wazi.