Vyombo vya habari vinahitaji nguvu ya kiuchumi kuwa huru – Spika Tulia
Na Paul Mallimbo
Dodoma: Spika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson amesema vyombo vya habari kuwa huru ni pamoja na kuwa na nguvu kiuchumi.
Dk. Tulia aliyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika siku ya pili kuelekea maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari Duniani (WPFD) ambayo huadhimishwa kila Mei 3 ya mwaka.
“Uhuru ni pamoja na wewe kuwa unajitosheleza na unaweza kusema kile ambacho kwa utalaam wako, ujuzi wako, na uanahabari wako unakutuma useme na siyo unasema kwa sababu mimi nimekuita kwenye mkutano halafu nikakulipa,”alionya.
Spika alikuwa akizungumzia madeni ambayo vyombo vya habari vinazidai taasisi za serikali kwa muda mrefu kutokana na matangazo ambayo yalichapishwa au kurushwa kwenye vyombo hivyo.
“Nafikiri katika kipindi hiki ambacho kimebaki kwa kweli inabidi nishirikiane na Mhe. Waziri wa Habari kwa zile taasisi hasa za serikali zinazodaiwa na vyombo vya habari zilipe na kwa hatua hiyo hiyo tutashirikiana na Waziri zile ambazo zinadaiwa tupate tu maandashi mahali ili kila wizara iwe inaulizwa wewe hapa umetenga sh ngapi kwa ajili ya kuvirudishia pesa vyombo vya habari ili viweze kufanya kazi kwa weledi. “ aliahidi.
Alisema kwa kuzingatia tunakoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, ili vyombo vya habari vitoe haki sawa na kuweka mzingira yanayofanana kwa wagombea wote, ni pamoja na vyombo hivyo kuwezeshwa kiuchumi ili viweze kufanya kazi zake kitaaluma.
Katika suala hilo hilo la uhuru wa vyombo vya habari, alihoji “je mtu mmoja anapokuwa anaandika habari yeye mwenyewe, yeye huyo huyo ndiyo mhariri, je hicho ni chombo cha habari”.
Pia, Spika Tulia aliwauliza waandishi wa habari kama mtu huyo mmoja anaweza kuwa chombo cha habari, kwa maana kuwa yeye ndiyo mwandishi, mhariri na mchapishaji. Alitahadharisha kuwa mtu mmoja anaweza kuliingiza taifa kwenye matatizo kama chombo chake hakitafuata msingi ya vyombo vya habari na kanuni za uandishi wa habari.
Alisema kumekuwa pia na tabia kwa baadhi ya watangazaji kujadili mambo binafsi kwenye vyombo vyao kwa muda mrefu, kitu ambacho ambacho hakina maslahi kwa umma, na kuhoji je hiyo ni habari.
Akizungumzia kuhusu Kauli Mbiu ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, isemayo uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi. Spika aliwataka waandishi wa habari kuandika habari za kuhabarisha umma kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inakipitia.
“Tunawategemea sana waandishi wa habari kwenye kuuhabarisha umma na kwenye kuuelimisha umma kuhusu hasa ni nini mabadiliko ya tabia nchi. Kwa sababu yako mambo ambayo tunayasema sisi ambao siyo wapeleka taarifa kama ninyi tunayasema kwa sura ambayo wakati mwingine wananchi wanachanganyikiwa hawaelewi kipi ndiyo mabadiliko ya tabia nchi na ni kipi ambacho kimekuwepo miaka yote,”.
Alisema ni lazima tutofautishe mazingira hayo mawili ili umma uelewa lipi ni tukio la kujirudiarudia na lipi ni tukio lilitokana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Nimefurahi kwamba nyinyi mmeweka kama sehemu ya yale ambayo mtakuwa mnajadiliana na mmetoa hii kama kauli mbiu mazingira yako hapo. Kwa hivyo naamini mtakapokuwa mnazungumza katika siku hizi mbili mtakubaliana namna ya kwenda na jambo hili ili sisi kama umma tupate uelewa kama watu wengine.”.
Dk. Tulia alisema hivi karibuni taifa limepitia changamoto ya mafuriko kwenye maeneo mbali mbali hapa nchini ambayo tumekuwa tukiyaita mabadiliko ya tabia nchi lakini yapo mengine ambayo wazee wenye miaka 80 na 90 ukiwaeleza wanakwambia wakati wana miaka minane tukio kama hili liliwahi kutokea.
“Sasa tutakuwa hatuelewei ni wakati gani tuseme haya ni mabadiliko ya tabia nchi na ni wakati gani tuone hili jambo linajirejea kwa sababu limewahi kutokea miaka ya nyuma.
Alisema Watanzania wanavitegemea vyombo vya habari kufanya tafiti na kuja na usahihi wa tukio lenyewe badala ya kukimbilia kuliita mabadilko ya tabia nchi.
Takwimu za watafiti zinaonyesha kuwa takribani watu milioni 16 nchini wanategemea rasilimali za Pwani kwa ajili ya kuendeshea maisha yao na hivyo uharibifu wa aina yoyote unaotokea una hatarisha maisha ya hawa watu milioni 16.
“Katika muktadha huu tunawategemea sana waandishi wa habari kutusaidia kuokoa haya mazingira ambayo na ninyi kwa kuona umuhimu wake, mmeweka kwenye kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Mwaka huu”, aliongeza.