Radio zatakiwa kuacha kuwa vijiwe vya soga

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura akisisitiza jambo kwa meneja na Mhariri Mkuu wa kituo cha redio ya Jembe FM kilichopo jijini Mwanza.

 

Februari 13, 2025: Baraza la habari Tanzania (MCT), limezionya redio kuacha kuwa vijiwe vya kupiga soga na badala yake zijikite kwenye majukumu yake muhimu ambayo ni kuhabarisha, kuburudisha na kuelimisha umma.

Aidha imekemea tabia ya baadhi ya wamiliki wa radio kuacha mara moja tabia ya kuajiri watangazaji kwa kufuata umaarufu wa mtu, badala ya taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji.

Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura aliyasema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani, ambayo huadhimishwa Febrauri 13, ya kila mwaka.

“Redio ziache kuwa vijiwe vya kujadiliana mambo binafsi na ya mtaani na badala yake zijikite kwenye taarifa zenye maslahi kwa umma, na maudhui yaliyofanyiwa utafiti unaolenga kuangazia na kujibu kero za jamii,” alisema katika taarifa yake.

Aidha katika taarifa hiyo, MCT imewaagiza watangazaji wa redio kufuata maadili ya utangazaji na kuzingatia matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili ili taarifa zinazotolewa kwa umma zieleweke kwa rika zote.

Katibu Mtendaji alihimiza umuhimu wa radio kutangaza maudhui yanayoihusu jamii kama elimu, afya, maendeleo yao, siasa, umuhimu wa jamii kuwashirikisha wanawake na masuala ya usalama.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Redio kwa Mabadiliko ya Tabia Nchi” ikiwa na lengo la kuhamasisha mijadala katika redio iliyojikita katika kutoa elimu, kuhamasisha mabadiliko endelevu na kuzishirikisha jamii katika majadiliano yanayoangazia mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa kutambua nguvu ya redio, MCT inatoa wito kwa redio kuandaa maudhui yatakayoelemisha wananchi kuhusu uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu ili jamii iweze kufuatilia mijadala na kufanya maamuzi sahihi  wakati wa kupiga kura.

Takwimu zinaonyesha kwamba, pamoja na kukua kwa teknolojia ya mawasiliano, redio ndio chombo kinachoaminiwa zaidi katika kusambaza taarifa kwa umma. Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (MICAS), hadi kufikia mwaka 2024, Tanzania ilikua na redio 247.