Waandishi wa Habari Waaswa: Epukeni Habari za Uzushi, Chuki Kipindi cha Uchaguzi

Wakati kikao cha wadau mbalimbali wa habari kikiendelea Arusha, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, amewataka waandishi wa habari kujiepusha na habari za uzushi, chuki, na matumizi ya lugha za chuki wakati wa kipindi cha uchaguzi. Kauli hiyo ameitoa Julai 28, 2025, akifungua rasmi mkutano wa siku mbili unaofanyika katika Hoteli ya Lush Garden, jijini Arusha.

 Sungura, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabaraza ya Habari Afrika Mashariki (EAPC), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC) na mjumbe wa Bodi ya Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA), amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi kwa jamii ili kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi.

 Mkutano huu muhimu, ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na International Media Support (IMS) na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida), unalenga kujadili na kupambana na tatizo la habari potofu na uzushi wakati wa uchaguzi. Ajenda kuu ni pamoja na kuunda kikosi kazi cha wadau kitakachoshughulikia masuala hayo na kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari, wadau mbalimbali wa uchaguzi, na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).

 Meneja wa Miradi wa International Media Support (IMS), Bi. Fausta Musokwa, amevitaka vyombo vya habari kuwa na waandishi maalum wa uchaguzi. Amesema hatua hii itasaidia kujenga ubobevu katika kuripoti masuala ya uchaguzi na kuepusha utoaji wa taarifa za uzushi, potofu, na zinazochochea chuki kabla, wakati, na baada ya uchaguzi.

 Katika mada iliyowasilishwa na Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), William Shao, kuhusu majukumu ya uhariri na mikakati ya chumba cha habari wakati wa uchaguzi, changamoto ya uhaba wa rasilimali fedha kwa vyombo vya habari iliibuliwa. Akichangia mada hiyo, Injinia Andrew Kisaka kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ameshauri vyombo vya habari kufikiri namna ya kutatua tatizo hili la uhaba wa fedha. Amehoji, “Iwapo Vyama vya siasa vinapewa ruzuku ili kugharamia uchaguzi, je, kwa nini isiwezekane kwa vyombo vya habari? Jiungeni na kuwa na mikakati ya pamoja katika kuwashirikisha wadau, ikiwemo serikali na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).”

 Mkutano huu unahudhuriwa na wajumbe kutoka asasi mbalimbali za habari, zikiwemo redio za jamii, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za serikali kama TCRA, Wizara ya Habari, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine cha Mwanza, Baraza la Habari Tanzania (MCT) na International Media Support (IMS). 

 Majadiliano yanaendelea Julai 29, 2025, na yanajumuisha mada kama vile matokeo ya awali ya utafiti wa Research ICT Africa (RIA) kuhusu habari potofu za uchaguzi, jukumu la ukaguzi wa ukweli wa habari (fact-checking) katika kukuza uadilifu wa michakato ya uchaguzi, na ujenzi wa mifumo ya ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kukabiliana na habari za uzushi. Pia, mmkutano huo utaunda timu ya kukabiliana na matukio ya habari za uzushi na kupanga mpango wa pamoja wa utekelezaji.