Warioba ahimiza kuandikwa habari za wananchi

Waziri Mkuu mstaafu na Mjumbe wa Bodi ya Udhamini ya Baraza la Habari Tanzania, Joseph Warioba akizungumza katika uzinduzi wa Bodi mpya ya Baraza.

 

Vyombo vya habari  nchini vimetakiwa kujikita zaidi kuandika habari za wananchi.

Akizindua Bodi mpya ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba,  amesema sasa inaelekea wananchi  wanafuatilia zaidi habari za vyombo vya nje  kulinganisha na za vyombo vya hapa nchini.

Hii siyo sifa alisema Warioba katika  uzinduzi huo uliofanyika katika hoteli ya Courtyard Jijini Dar es Salaam.

“Mimi napenda habari na madereva wangu wanajua …wakati wowote inapofikia kuwepo taarifa ya habari na nikiwa nipo kwenye gari, watafungulia ama TBC ama Radio One”, alisema.

Lakini sasa mambo yamebadilika . Badala ya kufungulia redio za hapa nchini watafungulia redio kama  DW, VOA ama vituo vingine vya radio vya nje, alisema.

Alisema kuwa aliwahi kuambiwa na raffik yake kuwa StarTV ina kipindi cha Dira ya Dunia  kinacoanza saa 3.00 usiku.

Hii maana yake ni nini? Warioba alisema inaelekea  vyombo vya habari vya ndani haviwatoshelezi wananchi.

Waziri Mkuu huyo mstaafu alisema kwa hali ya sasa vyombo vya habari vinaripoti zaidi kuhusu viongozi na msukumo umekuwa ni kutaka wananchi kuelimshwa.

Alitofautiana na mtazamo huo kwa kusema kuwa viongozi nao wanahitaji kujifunza kwa wananchi.

Aliendelea kuwa inaelekea vyombo vya habari vina woga na kwamba ule mtazamo  asilia wa uandishi wa habari kuwa “mbwa anapomuuma mtu si habari bali pale mtu anapomuuma mtu ni habari” hauzingatawi katika uandishi wa habari. Alisema pia habari za utafiti na uchunguzi zinazochochea na kuamsha mawazo zimedorora.

Katika hotuba yake fupi  na muhimu kwa mwelekeo wa vyombo vya habari nchini, alilisifia Baraza la Habari Tanzania  kwa kuleta maendeleo makubwa kwa  tasnia ya habari nchini.

Alikiri  kuwa Baraza limefanya kazi kubwa na anachohimiza yeye ni maboresho zaidi.

Alisema kuwa awali  kulikuwa na magazeti na  vituo vichache vya  vya redio na  televisheni haikupwepo lakini sasa  kuna vyombo vingi zaidi.

Pia alisema kuwa hakukuwa  na kanuni za maadili  wakati huo lakini sasa zipo  zinazohusu vyombo aina mbalimbali vya habari.

Warioba   aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ya Maadili ya MCT na  hivi sasa ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, aliwakabidhi wajumbe wa Bodi mpya ya Baraza vitendea kazi ambavyo ni pamoja na Katiba ya  Baraza.

Wanachama waliokuwepo katika uzinduzi wa Bodi  ni pamoja na Rais mpya Jaji mstaafu Juxon Mlay na Makamu Rais Yusuf Khamis. Wengine ni Happiness Nkya, Edda Sanga, Bakari Machumu na Dk. Joyce Bazira

Wajumbe ambao  hawakuwepo na kutoa udhuru ni pamoja na  Tido Mhando mwenyekiti mpya wa Kamati ya Maadili,  Teddy Mapunda  na Anna Henga.

Hii ni  Bodi ya tisa ya Baraza. Wajumbe wa Bodi hiyo walichaguliwa katika mkutano wa  mwaka  wa  MCT uliofanyika Tanga, Septemba 28,2020.