TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Dar es Salaam, Alhamis, Septemba 19, 2024

 Majaji saba wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) wamehitimisha kazi ya kutathmini ubora na weledi wa kazi zipatazo 1,135 na kuwateua waandishi wa habari 72 watakaoingia katika kinyang’anyiro cha kumtambua mshindi wa kwanza, wa pili na wa tatu na mshindi wa jumla.

Kati ya waandishi wa habari 72, wanaume ni 45 (sawa na 62.5%) na wanawake 27 (sawa na 37.5%). Kati ya wateule hao, wateule 14 (19%) wanatoka katika runinga; 13 (18%) wanatoka vyombo vya mtandaoni, redio 20 (28%) na wateule 25 (35%) wanatoka kwenye magazeti.

Wateule wamepatikana kwa kukidhi vigezo vya ubora ambavyo ni pamoja na ukweli, usahihi, uanuai, haki, kina, utafiti, ubunifu, uvumbuzi, upekee, uchambuzi, uwajibikaji, ufichuaji maovu, uadilifu, uwasilishaji unaoeleweka na uchunguzi. Ifahamike pia kwamba vigezo maalum vilitumika kuzingatia aina tofauti ya vyombo vya habari kama vile redio, televisheni, magazeti na habari za mitandaoni.

Kabla ya kutaja majina ya wateule hao 72 ni muhimu ifahamike kwamba kinyang’anyiro cha kumtambua mshindi wa kwanza, wa pili na wa tatu na mshindi wa jumla kwa makundi 20 ya kushindaniwa kitakuwa siku ya jumamosi, tarehe 28 Septemba, 2024 ambapo mgeni rasmi katika siku ya kilele cha kinyang’anyiro atakuwa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge Duniani, Dkt Tulia Akson.

Mgeni rasmi ndiye atakayemkabidhi tuzo mshindi wa jumla atakayewapiku kwa umahiri waandishi wengine 71 katika hafla itakayofanyika katika ukumbi wa Aga Khan Daimond Jubilee, Dar es Salaam. Hii itakuwa ni mara ya 15 kutoa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Tanzania.

Moja ya jambo la kipekee katika kilele cha kinyang’anyiro hicho ni pamoja na kusikia kutoka kwa jopo la majaji kuhusu viwango vya uandishi wa habari za magazeti, redio, televisheni na mitandaoni  kwa habari zilizohusu uwekezaji wa kampuni ya DP world katika bandari za Tanzania, habari kuhusu Ngorongoro na wamasai na kuhusu maporomoko ya Hanang.

Jambo la pili la kipekee ni kumshuhudia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry Silaa akizindua Jarida la Tuzo na Tuzo magazine ambayo yanajikita kuhamasisha umahiri katika sekta mbalimbali Tanzania na nje ya Tanzania. Kwa kuanzia majarida hayo, moja la Kiswahili na lingine la Kiingereza yatabeba maudhui ya tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Tanzania (EJAT).

Moja ya maudhui katika majarida yote mawili ni simulizi ya maisha ya wateule wote. Kazi ya kuandika simulizi hizo inaanza leo, hivyo wateule wote wawe tayari kufikiwa na waandishi wa Jarida la Tuzo wakati wowote kuanzia sasa. Maudhui mengine ni ya wafadhili wa tuzo ambao simulizi zitahusu mchango wao katika kubadilisha maisha ya watu ikiwemo kukuza na kujenga tasnia ya habari.

Aidha ikumbukwe kuwa kwa mara ya kwanza kazi za kihabari kwa EJAT 2023 zimeongezeka hadi 1,135 kutoka kazi 893 za EJAT 2022. EJAT 2020 kazi zilikuwa 396 na EJAT 2021 kazi zilikuwa 608.

Waandishi wa habari wa mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka huu waliongoza kwa kuwasilisha kazi 290, wakifuatiwa na mkoa wa Arusha uliokuwa na kazi 81, Mwanza kazi 74, Iringa ilishika nafasi ya nne kwa kuwa na kazi 72, wakati mkoa wa Mtwara ulishika nafasi ya tano kwa kuwa na kazi 49.  Kwa upande wa Zanzibar, kazi zilizopokelewa ni kutoka Kaskazini Pemba (36) Pemba Kusini (43) na Mjini Magharibi (29).

Dirisha la kupokea kazi za waandishi wa habari lilifunguliwa tangu Novemba 15,  mwaka jana na kufungwa Februari 28, mwaka huu. Kazi ya kuchambua na kutathmini ubora wa kazi za kihabari za mwaka 2023 ilianza tarehe 7 hadi 15 baada ya Naibu msajili wa mahakama kuu, Morogoro, Mheshimiwa Fadhil Mbelwa kuwaapisha majaji.

Jopo la Majaji liliongozwa na Halima Shariff, katibu wake Dkt Egbert Mkoko na majaji wengine wakiwa ni pamoja na Ndugu Mkumbwa Ally, Eshe Muhiddin, Jeniffer Sumi, Halima Msellemu na Absalom Kibanda.

Jopo lilichaguliwa na wakuu wa taasisi za kihabari zinazounda kamati ya maandalizi ya EJAT kwa kuzingatia uadilifu, ujuzi na uzoefu katika uandishi wa habari, uwezo wa kuchambua na kutoa tathmini sahihi, uelewa wa mabadiliko ya kidigitali, uzoefu wa kimataifa au wa kijamii.

Aidha, jopo la majaji lilizingatia uwiano wa kizazi kipya na cha zamani, waliopo kazini na waliostaafu, wabobezi wa maudhui mahsusi, usawa wa kijinsia, uwakilishi wa Zanzibar na Tanzania Bara na uwakilishi wa aina ya vyombo vya habari (magazeti, redio, luninga na  mitandao).

Mbali na Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari, mchakato wa kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Maisha ya Mafanikio Katika Uandishi wa Habari (LAJA) 2024 unatarajiwa kuhitimishwa leo na wakuu wa kamati ya maandalizi. Tuzo hii humtambua mwandishi ambaye katika maisha yake ametoa mchango mkubwa katika kuiendeleza tasnia ya habari.

Taasisi zinaounda Kamati ya Maandalizi ni Wakfu wa Vyombo vya Habari (TMF), Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Jukwaa la Wahariri (TEF), HakiElimu, Umoja wa Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Sikika, Misa –  Tan  na Twaweza.

Sasa nimalizie kwa kusoma orodha ya wateule wa EJAT 2023 pamoja na vyombo vyao:

 

NA. JINA JINSIA CHOMBO MKOA
1 Thomas Masalu Lunyalo M Mazingira FM Mara
2 Abdallah Bakari Nassoro M Nipashe Mtwara
3 Jacob Mogesi Musenda M The Citizen Dar es Salaam
4 Marco Maduhu M Shinyanga Press Club Shinyanga
5 Salum Vuai Issa M Zanzibar Leo Zanzibar
6 Jackline Victor Kuwanda F The Chanzo Dodoma
7 Stanslaus Lambert M Swahili 360 Dar es Salaam
8 Zacharia Nyamoga M IPC Mkombozi TV Iringa
9 Irene Mwakalinga F TBC1 Iringa
10 Said Ally Sindo M Storm FM Geita
11 Joshua Stephen M Nukta Dar es Salaam
12 Samweli Mpogole M Highlands FM Mbeya
13 Shekha Suleiman F ZBC Pemba
14 Abel Kilumbu M Dar 24 Dar es Salaam
15 Khamis Mohamed M Zanzibar Leo Zanzibar
16 Abdiel Jumanne Siffi M UFM Dar es Salaam
17 Julius Maricha Maricha M The Citizen Dar es Salaam
18 Eliya Solomon M Mwanaspoti Dar es Salaam
19 Huwaida Nassor Moh’d F As Salaam FM Zanzibar
20 Rehema Evance Mwaikema F UTV Simiyu
21 Philip Mwihava Mwihava M Clouds FM Dar es Salaam
22 Zourha John Malisa F Mwananchi Dar es Salaam
23 Linus Ananias Gamarwa M TBC Dodoma
24 Catherine Sekibaha F Pangani FM Pangani Tanga
25 Herieth Makwetta F Mwananchi Dar es Salaam
26 George Helahela M Mwananchi Dar es Salaam
27 Esau Ezra Ng’umbi M Nukta Habari Dar es Salaam
28 Benson Eustace Jacob M UTV Kagera
290 Mariamu Ally Abdallah F Pangani FM Tanga
30 Adam Gabriel Hhando M CG FM Tabora
31 Sanula Renatus Athanas M Nipashe Dar es Salaam
32 Elizabeth Edward Kusekwa F Mwananchi Dar es Salaam
33 Pamela Nasphory Chilongola F Mwananchi Dar es Salaam
34 Rodgers Simon M ITV Dar es Salaam
35 Mukrim Mohamed Khamis M KTV TZ Online Zanzibar
36 Ephrahem Edward Bahemu M Mwananchi Dar es Salaam
37 Mkwaji Reuben Masatu F UTV Dar es Salaam
38 Lukelo Francis Haule M The Chanzo Dar es Salaam
39 Benjamin Mzinga M ITV Dar es Salaam
40 Dickson Shukran Kanyika M RFA Njombe
41 Hamisi Makungu Hamisi M Pangani FM Pangani Tanga
42 Halfan Chusi M Nipashe Dar es Salaam
43 Kelvin Paul Matandiko M Mwananchi Dar es Salaam
44 Waryoba Musa Waryoba M Montessory Tanzania Mwanza
45 Anna Peter  Mbuthu F TBC Arusha
46 Egan Salla M BBC Dar es Salaam
47 Imma Rashid Mbuguni M Majira Online Dar es Salaam
48 Haika E. Kimaro F The Citizen Mtwara
49 Margareth Msafiri Geddy M TBC Safari Dar es Salaam
50 Yohana Chance Challe M Mwanaspoti Mbeya
51 Mgongo Kaitira Mafuru M Mwananchi Mwanza
52 Mercy Yasin Mbaya F UTV Dar es Salaam
53 Imani Raphael Makongoro F Mwananchi Pwani
54 Fatma Abdallah Chikawe F UTV Dar es Salaam
55 Brown Benny Mbwawa M Wasafi FM Mbeya
56 Ayoub Stanley Nyondo M Shamba FM Iringa
57 Warioba Igombe Warioba M Uhuru Mara
58 Salome Gregory Sumbya F The Citizen Dar es Salaam
59 Veronica Natalis Mataba F DW Swahili Arusha
60 Saa Mbwana Zumo F Pangani FM Pangani Tanga
61 Said Ali Ngamba M Uyui FM Tabora
62 Lugendo Madege M UFM Dar es Salaam
63 Anna Potinus F Mwananchi Mwanza
64 Christina Mwakangale F Nipashe Dar es Salaam
65 Rauhiya M Shaban F Bomba FM Zanzibar
66 Hazla Omary Quire F The Tanzania Times Arusha
67 Lucy Patrick Samson F Nukta Dar es Salaam
68 Mohamed Hammie Rajabu M Habari Leo Dar es Salaam
69 Amina Deogratias Semagogwa F Radio Kwizera Kigoma
70 Hellen Nachilongo Mkisi F The Citizen Dar es Salaam
71 Alfred Bulahya Jakuba M Dodoma FM Dodoma
72 Waziri Iddi Suka M Tumaini TV Dar es Salaam

Hongereni sana kuingia katika kinyang’anyiro cha Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2023.

Ernest S. Sungura

Mwenyekiti

Kamati ya Maandalizi ya EJAT 2023