Siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari Duniani 2025

Katibu Mtendaji wa MCT Ernest Sungura (kulia) akizungumza na Programme Director wa Wajibika Programme na Oxford Policy Management Adelaide Addo-fening (kushoto) walipokutana katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari (WPFD) yanayofanyika Jijini Arusha. Katikati yao ni Mwandishi wa Habari Mkongwe Rose Haji Mwalimu.
Arusha: Aprili 28, 2025. Baraza la Habari Tanzania (MCT), likiwakilishwa na Katibu Mtendaji, Ernest Sungura na baadhi ya wafanyakazi wa Baraza, limeungana na wadau mbalimbali wa vyombo vya habari nchini, katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo ya Habari duniani.
Maadhimisho hayo kitaifa yanafanyika jijini Arusha ambapo kaulimbiu yake ni Uhabarishaji kwenye dunia mpya: Mchango wa Akili Unde kwenye uhuru wa vyombo vya habari, ambayo inatoa changamoto kwa waandishi, wamiliki wa vyombo vya habari na serikali kuhakikisha kwamba Akili Unde inaibua fursa kwa uhuru wa vyombo vya habari na inasaidia watu haki ya kupata habari sahihi.
MCT, kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Kituo cha Haki za Binanamu (LHRC), wameandaa mjadala maalumu, unaolishikisha Bunge la Tanzania, kujadili Mfumo wa Kisheria na Udhibiti na Wajibu wa Bunge Katika Uhuru wa Vyombo vya Habari nchini.
Maadhimisho hayo pia yanatoa nafasi kwa wadau wa sekta ya habari, mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia kujadili masuala muhimu yanayohusu habari na changamoto zinazohusiana na teknolojia.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.