Zingatieni Maadili ya Uandishi wa Habari za Uchaguzi - MCT

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Zingatieni Maadili ya Uandishi wa Habari za Uchaguzi – MCT

 26 Novemba, 2024, Dar es Salaam,

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limekuwa likifuatilia mwenendo wa uandishi wa habari za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kabla, wakati wa kampeni na litafanya hivyo siku na baada ya kupiga kura kesho Jumatano, Novemba 27, mwaka huu.

Baadhi ya vyombo vya habari ambavyo kwa namna moja au nyingine vimekuwa vikikiuka maadili na weledi, MCT imekuwa ikiwasiliana na wahariri wa vyombo husika kuwakumbusha kuandika au kutangaza habari zake kwa weledi na kufuata misingi na maadili ya uandishi wa habari.

MCT inawapongeza wahariri ambao wamekuwa wakizingatia misingi na maadili ya uandishi wa habari kwani kwa kufanya hivyo wamekuwa wakitimiza wajibu wa kuwapasha wananchi habari sahihi na za kina zitakazowasaidia kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Kwa mujibu wa Katiba ya MCT ya 1995, kipengele namba 3 (b), wanachama wa MCT wamekipa chombo walichokiunda mamlaka kuisimamia tasnia ya habari na kuhakikisha uandishi wa habari wenye weledi na unaofuata maadili, “Baraza litasimamia waandishi wa habari, wahariri, watangazaji, wazalishaji vipindi, wamiliki na wote wanaohusika katika tasnia ya habari kuzingatia weledi wa hali ya juu na kanuni za maadili ya habari,”

Ni kwa mamlaka hayo, MCT linavikumbusha vyombo vya habari kuzingatia maadili na weledi wakati wote vinaporipoti kauli, ziwe za viongozi wa kisiasa, kidini, kijamii au za wapambe wao, na visikubali kugeuzwa vipaza sauti au wapiga debe katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Aidha, MCT inavikumbusha vyombo vya habari umuhimu wa kuzisoma kanuni na sheria za uchaguzi zinazotolewa na mamlaka husika ili kutojiingiza kwenye mgogoro wa kikanuni na kisheria.

Mfano wa kanuni hizo ni Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (maudhui ya utangazaji kwa redio na televisheni), za mwaka 2018 pamoja na mabadiliko yake ya mwaka 2022, vifungu namba 19 (a) vinazungumzia suala la fursa sawa kwa vyama vinavyoshiriki kwenye uchaguzi.

Kifungu namba 19 (b): kinazungumzia fursa sawa kwa wagombea na kuripoti kwa usawa taarifa zao na kifungu namba 19 (f): kinazungumzia kuepuka kuegemea upande mmoja.

Kanuni za Maadili ya Uandishi wa Habari toleo la 2020, kipengele namba 6.0 kinazungumzia umuhimu wa uandishi wa habari unaozingatia haki na usawa, wakati kipengele 7.0 kinazungumzia kupewa haki ya kujibu.

Baraza linahimiza vyombo vya habari vya Tanzania vikatae kushiriki kwa namna  yoyote ile katika vitendo vinavyoashiria upendeleo wa kisiasa, kijinsia na pia vitendo vinavyochochea uhasama katika Taifa kwa kusambaza uzushi, matusi, udini, vitisho na chuki huku vikizingatia na kukumbuka madhara yatakayotokana na vyombo vya habari kutozingatia kanuni za maadili ya uandishi wa habari.

 

Ernest  S. Sungura
Katibu Mtendaji